Featured Kitaifa

JKT YAIMARISHA JUHUDI ZA KUINUA KILIMO KUPITIA ELIMU NA TEKNOLOJIA

Written by Alex Sonna

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-Dodoma

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limeeleza kuwa litaendelea kuwafikia wananchi kwa kutoa elimu ya kilimo cha kisasa, ufugaji na uvuvi hata baada ya kuhitimishwa kwa Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane, likisisitiza kuwa jukumu lake ni kujenga jamii yenye maarifa, uzalishaji mkubwa na uchumi imara.

 Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele, amesema JKT imejipanga kuhakikisha elimu inayotolewa kwa wananchi haibaki kuwa ya maonesho pekee, bali inaendelea kufikishwa katika maeneo mbalimbali nchini kupitia wataalamu wa jeshi hilo ili kuongeza tija katika sekta ya kilimo.

Akizungumza baada ya kutembelea mabanda ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, Meja Jenerali Mabele amesema  JKT imeendelea kubadili mtazamo wa wananchi kwa kuwaonesha kuwa kilimo, ufugaji na uvuvi vinaweza kufanyika kwa njia za kisasa na kuleta matokeo makubwa ya kiuchumi.

Amesema  maonesho hayo yamekuwa darasa la wazi kwa wananchi kujifunza teknolojia mpya za uzalishaji, matumizi bora ya ardhi, mbinu za kuongeza thamani ya mazao na namna ya kutumia rasilimali walizonazo kwa ufanisi ili kuongeza kipato na kuimarisha usalama wa chakula.

“Lengo letu si kuishia kushiriki maonesho. Tunataka elimu tunayotoa iwafikie Watanzania wengi zaidi na iwe sehemu ya maisha yao ya kila siku. Tutazidi kuwa karibu na wananchi kupitia mafunzo na ushauri wa kitaalamu ili kuongeza uzalishaji na kuinua uchumi wa familia na taifa,” amesema  Meja Jenerali Mabele.

Amebainisha kuwa wataalamu wa JKT wataendelea kuwapa wakulima, wafugaji na wavuvi mbinu bora za uzalishaji, matumizi ya teknolojia za kisasa pamoja na usimamizi sahihi wa shughuli zao ili kuzalisha kwa tija zaidi.

Meja Jenerali Mabele amesema  banda la JKT limeendelea kuwa miongoni mwa yaliyovutia idadi kubwa ya wageni katika maonesho hayo, ambapo wananchi wamekuwa wakipata fursa ya kujionea bidhaa zinazozalishwa katika mashamba na miradi ya jeshi hilo pamoja na kupata elimu ya moja kwa moja kutoka kwa wataalamu.

Ameongeza kuwa ushiriki wa JKT katika Maonesho ya Nane Nane hauishii Dodoma pekee, bali unaendelea katika kanda mbalimbali nchini ikiwemo Arusha, Morogoro, Mbeya, Lindi na Simiyu, hatua inayowezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na elimu na teknolojia zinazotolewa na jeshi hilo.

Aidha, amewataka wananchi kutumia fursa ya maonesho hayo kutembelea banda la JKT ili kujifunza mbinu za kisasa za uzalishaji na kufahamu fursa mbalimbali zinazotolewa na jeshi hilo katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi, akisisitiza kuwa maarifa ndiyo msingi wa kuongeza uzalishaji na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.

About the author

Alex Sonna