Featured Kitaifa

MWAKIBINGA: TUNAHITAJI MKULIMA APATE THAMANI HALISI YA NGUVU ALIYOIWEKEZA

Written by Alex Sonna

Mkurugenzi wa Huduma Saidizi, Wakala wa Vipimo (WMA), Christopher Mwakibinga, akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 4,2026  katika Banda la WMA wakati wa Maonesho ya 49 ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Alban Kihulla.

*Na WMA – Dodoma*

Mkurugenzi wa Huduma Saidizi, Wakala wa Vipimo (WMA), Christopher Mwakibinga, amesema kuwa Wakala hiyo inaendelea kutekeleza jukumu lake la kulinda haki za wakulima na watumiaji wa huduma mbalimbali kwa kuhakikisha vifaa vya vipimo vinavyotumika katika sekta ya kilimo na uzalishaji vinahakikiwa kwa mujibu wa sheria.

Ameyasema hayo Agosti 4, 2026 alipokuwa akizungumza katika Banda la WMA kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Alban Kihulla, wakati wa Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea jijini Dodoma.

Amesema shughuli za Wakala wa Vipimo zimehusishwa moja kwa moja na mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo, ambapo taasisi hiyo huhakiki mita za maji zinazotumika katika kilimo cha umwagiliaji ili kuhakikisha wakulima na watumiaji wa huduma hiyo wanalindwa.

Aidha, amesema WMA pia huhakiki mita za umeme zinazotumika viwandani kwa lengo la kuwalinda watumiaji wa umeme pamoja na wamiliki wa viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao ya kilimo.

Pia, amebainisha kuwa WMA pia huhakiki mizani inayotumika katika ununuzi wa mazao ya kimkakati yakiwemo korosho, pamba, tumbaku na mengineyo, ili kuhakikisha wakulima wanapata thamani halisi ya mazao yao kulingana na nguvu na gharama wanazowekeza katika uzalishaji.

Ameongeza kuwa WMA inaendesha kampeni mbalimbali za kuwaelimisha na kuwawezesha wakulima kuhakikisha wanatumia mizani iliyohakikiwa ili kupata haki yao katika biashara ya mazao.

Aidha, amebainisha Kuwa WMA inapinga matumizi ya utaratibu unaojulikana kama lumbesa, akieleza kuwa mfumo huo unaweza kumnyima mkulima thamani halisi ya mazao yake.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa majukumu ya Wakala wa Vipimo unaendana na kaulimbiu ya Maonesho ya Nane Nane mwaka huu inayosema, “Tambua Soko; Ongeza Tija Kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”

About the author

Alex Sonna