Malkia wa tenisi duniani, Serena Williams, anatarajiwa kurejea rasmi kwenye mashindano ya kitaaluma baada ya takribani miaka minne nje ya mchezo huo, huku akitarajiwa kushuka dimbani Jumanne katika mashindano ya Queen’s Club jijini London.
Mmarekani huyo mwenye mataji 23 ya Grand Slam amepewa nafasi ya wildcard katika mchezo wa wanawake wawili (doubles), ambapo atacheza sambamba na nyota chipukizi wa Canada, Victoria Mboko. Wawili hao watamenyana na Erin Routliffe na Nicole Melichar-Martinez katika mechi ya maandalizi kuelekea mashindano ya Wimbledon.
Serena alionekana mara ya mwisho kwenye mashindano ya US Open mwaka 2022 kabla ya kueleza nia ya kuhitimisha safari yake ya tenisi. Hata hivyo, sasa ameamua kurejea uwanjani, akisema anatamani watoto wake washuhudie akicheza tena katika kiwango cha ushindani wa juu.
Licha ya kurejea kwake, Serena amesema bado hajafanya uamuzi wa mwisho kuhusu kushiriki mashindano ya mchezo mmoja mmoja (singles), ingawa hajafunga mlango wa uwezekano huo.
Baada ya Queen’s Club, nyota huyo anatarajiwa kushiriki pia mashindano ya Berlin Open, hatua inayozidi kuongeza hamasa kwa mashabiki wanaosubiri kuona kama atarejea kwa ubora uliomtambulisha kama mmoja wa wachezaji bora zaidi katika historia ya tenisi.