Na Mwandishi Wetu
Kikosi cha taifa cha Brazil kimepata nafuu ya moyo baada ya taarifa za kitabibu kuthibitisha kuwa nyota wake Neymar Jr. anaendelea vizuri na mchakato wa kupona jeraha la nyama ya ndama (calf), hatua inayoongeza matumaini ya kurejea kwake uwanjani mapema.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Brazil (CBF), vipimo vya MRI vilivyofanyika hivi karibuni vinaonyesha maendeleo mazuri katika tiba ya mshambuliaji huyo, ambaye kwa sasa yupo chini ya uangalizi maalumu wa madaktari wa timu ya taifa.
Neymar alipata jeraha la kiwango cha pili kwenye misuli katikati ya mwezi Mei, hali iliyomlazimu kukosa mechi za kirafiki dhidi ya Panama na Misri. Awali madaktari walikadiria angekaa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki mbili hadi tatu ili kupata nafuu kamili.
Licha ya maendeleo hayo, bado haijathibitishwa kama nahodha huyo wa zamani wa Brazil atakuwa fiti kwa ajili ya mechi ya ufunguzi dhidi ya Morocco, huku benchi la ufundi likiendelea kufuatilia hali yake kwa karibu kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.
Kurejea kwa Neymar kutakuwa habari njema kwa Brazil, ambao wanaendelea kutafuta njia ya kurejesha hadhi yao ya kimataifa baada ya kushindwa kutwaa ubingwa wa dunia tangu mwaka 2002. Mashabiki wengi wanaamini uzoefu na ubora wa nyota huyo vinaweza kuwa silaha muhimu katika safari ya timu hiyo.
Brazil wanatarajiwa kuanza kampeni yao kwa mchezo dhidi ya Morocco kabla ya kuvaana na Haiti Juni 19 mjini Philadelphia na baadaye Scotland Juni 24 mjini Miami katika hatua ya makundi.