Na.Alex Sonna,Mzalendo blog -DODOMA
Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) umeeleza kuwa matumizi ya vipimo sahihi yana mchango mkubwa katika kupanga sera na kufanya maamuzi sahihi ya maendeleo ya kiuchumi nchini.
Akizungumza na watumishi wa wakala huo jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka WMA, Francis Olwero, amesema takwimu zinazotokana na vipimo sahihi husaidia serikali kupanga sera zenye tija katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, kilimo, viwanda na huduma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani ambayo huadhimishwa Mei 20 kila mwaka.
Olwero amesema matumizi ya vipimo visivyo sahihi yanaweza kuathiri ukusanyaji wa taarifa muhimu za uzalishaji na biashara, hali inayoweza kusababisha upangaji usio sahihi wa mipango ya maendeleo na matumizi mabaya ya rasilimali.
“WMA itaendelea kutoa elimu kwa wananchi na wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kutumia mizani na vipimo vilivyothibitishwa ili kujenga uchumi wenye ushindani, uwazi na unaolinda maslahi ya walaji pamoja na wafanyabiashara.”amesema Bw.Olwero
\




