Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 14, 2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Tanzania imeendelea kuthibitisha ubora wake katika sekta ya uchumi wa buluu baada ya kuendelea kuwa kinara wa uzalishaji wa mwani barani Afrika, hatua inayotajwa kuchochea ukuaji wa kipato kwa maelfu ya wananchi wanaojishughulisha na kilimo hicho hususan maeneo ya ukanda wa pwani na visiwani Zanzibar.
Hayo yamesemwa leo Mei 14, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema kuwa takwimu zinaonesha kuwa hadi Aprili 2026, Tanzania imezalisha tani 132,479.29 za mwani zenye thamani ya shilingi trilioni 13.9, ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na tani 88,615.2 zenye thamani ya shilingi bilioni 9.3 zilizozalishwa katika kipindi kama hicho mwaka 2024/2025.
“Ongezeko hilo la asilimia 49.5 linaashiria mafanikio makubwa ya juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta ya mwani ambayo imeendelea kuwa tegemeo muhimu la ajira, mapato ya kaya pamoja na chanzo cha fedha za kigeni.”amesema Dkt.Bashiru
Aidha,amesema kuwa maboresho ya teknolojia za uzalishaji pamoja na kuongezeka kwa uelewa kwa wakulima yameendelea kuongeza uzalishaji na ubora wa mwani unaolimwa nchini.
Tanzania imekuwa ikifanya jitihada za kuendeleza uchumi wa buluu kwa kuwekeza zaidi katika sekta za bahari na rasilimali zake, huku mwani ukiwa moja ya mazao yanayochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya wananchi wa maeneo ya pwani.