Featured • Kitaifa

WAANDISHI WA HABARI WAPIGWA MSASA UTAYARISHAJI VIPINDI VYA WATOTO

Written by Alex Sonna

 

 

Na WMJJWM – Dar es Salaam

Waandaaji wa vipindi vya watoto wamehimizwa

kutumia taaluma zao na lugha rafiki kwa watoto na vijana pamoja na

kuzingatia maadili ya taaluma ya Habari katika kuandaa maudhui yenye

ubora yatakayochangia ukuaji na maendeleo ya mtoto katika jamii.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa Programu ya malezi na familia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Victor RugalabamuMei 8, 2026 

wakati wa kuhitimisha mafunzo maalum yaliyoandaliwa na Wizara hiyo kwa

kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia

watoto (UNICEF) kwa lengo la kuwajengea uwezo waandaaji wa vipindi wa radio za

jamii, Televisheni na Mitandao ya Kijamii katika kutengeneza maudhui

yanayofundisha, kuburudisha na kuhamasisha maadili mema kwa watoto.

Victor amesema, kupitia mafunzo hayo, Wizara inatarajia kuona vipindi vitakavyorushwa kupitia vyombo vya habari vinatoa mafunzo ya

maadili mema kwa kizazi cha sasa na kijacho pia vinahamasisha

malezi mazuri ndani ya familia na kuwasaidia watoto na vijana

balehe kukua katika mazingira salama, yenye upendo na ulinzi.

Kwa upande wake Mwezeshaji wa mafunzo hayo,

Sabrina Majikata kutoka Shirikia Lisilo la Kiserikali la ICS amesema

mafunzo yamejikita kuwawezesha Waandishi wa Habari katika kutayarisha

vipindi bora na kuzungumza kwa ufasaha katika nguzo tatu ambazo ni

namna ya mzazi kumjali, kumtunza na

kuzungumza na mtoto ili aweze kubaini changamoto zinazoweza kuathiri

maendeleo yake.

“Mwandishi wa habari anapokuwa na uelewa kuhusu ukuaji wa watoto

na changamoto zinazowakabili pamoja na vijana balehe, anakuwa

na uwezo mkubwa wa kutengeneza maudhui yenye manufaa kwa jamii. 

Kupitia mafunzo haya, tumesisitiza umuhimu wa kuandaa vipindi

vinavyolinda maslahi ya mtoto, vinavyotoa elimu sahihi na vinavyochochea mawasiliano mazuri ndani ya familia”. Amesema Sabrina

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia

Watoto (UNICEF) Alice Mwiru ambaye

ni Mtaalamu wa mabadiliko ya tabia za jamii, amehimiza waandishi wa habari kuongeza ubunifu na uwajibikaji katika utayarishaji wa vipindi vya Watoto, amesisitiza kuwa UNICEF itaendelea kushirikiana na

Serikali kuboresha maudhui yanayohusu watoto ili kuhakikisha haki za mtoto na masuala yao yanapewa kipaumbele katika majukwaa ya habari.

Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Godliver Thomasi kutoka Jamii Forums amesema mafunzo hayo yamempa mwanga zaidi namna ya kuandaa vipindi husika.

“Mafunzo haya yamenipa uelewa mpana kuhusu namna ya kuandaa maudhui

yanayowagusa watoto na vijana kwa njia sahihi na yenye kujenga. Nimejifunza umuhimu wa kutumia lugha rafiki, kuzingatia hatua za

ukuaji wa mtoto pamoja na kuandaa vipindi vinavyofundisha na kuburudisha kwa wakati mmoja. Kupitia elimu hii, ninaamini nitakuwa sehemu ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii kupitia kazi yangu ya uandishi wa habari”.

 

About the author

Alex Sonna