Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Wabunge wameipongeza Mpango wa Bajeti uliowasilishwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2026/27, wakieleza kuwa umeweka mkazo mkubwa katika kuboresha elimu ya ufundi na mafunzo ya stadi, hatua itakayosaidia kuongeza fursa za ajira kwa vijana nchini.
Wakichangia mjadala bungeni leo,Mei 7,2026 bungeni, wabunge hao wamesema mpango huo unaonesha dira ya Serikali katika kuimarisha elimu inayolenga soko la ajira, hususan kupitia ujenzi na upanuzi wa vyuo vya ufundi na taasisi za mafunzo ya stadi.
Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Viti Maalum, Asha Juma Ferouz (CCM) ameipongeza Wizara ya Elimu pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuongeza mgao wa fedha katika sekta ya elimu, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kukuza rasilimali watu na kuongeza ufanisi wa elimu nchini.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Elimu,Utamaduni na Michezo amesema uamuzi wa Serikali wa kupanua vyuo kutoka 80 hadi 145 utaongeza nafasi kwa vijana wengi kupata mafunzo ya ufundi na stadi za kazi, jambo litakalosaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana na kuongeza uzalishaji katika sekta mbalimbali za uchumi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum, Dkt Zeyana Abdallah Hamad (CCM) amesema Rais Samia ameonesha uongozi imara na uungwana kwa kuhakikisha sekta ya elimu inapewa kipaumbele kupitia ongezeko la bajeti, akieleza kuwa uwekezaji huo ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa.
Dkt Zeyana ambaye anawakilisha kundi la wasomi amesema hatua ya Serikali kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya vitendo itasaidia kuzalisha vijana wenye ujuzi unaohitajika sokoni, hivyo kuongeza ushindani na tija katika uchumi wa nchi.