Kampuni ya Qualcomm Incorporated leo imetangaza uteuzi wa kampuni changa au startups 10 kwa mwaka wa nne wa Mpango wa Ushauri wa Qualcomm® Make in Africa.
Mpango huo ni sehemu ya jukwaa la ubunifu la kampuni hiyo barani Afrika, ukilenga kukuza maendeleo ya teknolojia za kisasa kwa kuwajengea uwezo wabunifu chipukizi kupitia mafunzo na ushauri wa kitaalamu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, programu hiyo inalenga zaidi teknolojia za mawasiliano na uchakataji wa kisasa ikiwemo Edge AI/ML, Intaneti ya Vitu (IoT), pamoja na majukwaa ya maendeleo ya akili bandia kwa kushirikiana na Arduino.
Katika hatua ya mwisho ya mpango huo, kampuni moja bora itapata ruzuku kutoka mfuko wa *Qualcomm for Good, huku kila mshiriki atakayekamilisha programu hiyo akitarajiwa kupata posho ya dola za Marekani 5,000.
Aidha, washiriki watapata rasilimali mbalimbali ikiwemo mwongozo wa kubuni bidhaa kwa kutumia majukwaa ya Arduino AI, ushauri wa biashara, pamoja na upatikanaji wa wataalamu wa uhandisi. Pia watapatiwa elimu ya miliki bunifu kupitia programu ya L2Pro Africa.
Washiriki watapata majukwaa ya Arduino yenye uwezo wa edge-AI bila malipo, pamoja na ushauri wa kiufundi na biashara. Fabio Violante wa Arduino alisema kuwa vifaa kama Arduino® UNO™ Q vinawawezesha waanzilishi kubadilisha mawazo kuwa mashine janja kwa haraka.
Kwa mwaka huu, kampuni 10 zilichaguliwa kutoka zaidi ya maombi 1,200 yaliyotoka katika nchi zaidi ya 45 za Afrika, huku sekta mbalimbali zikihusishwa ikiwemo kilimo, elimu, miji janja, usafiri wa magari ya umeme na teknolojia saidizi.
Kampuni zilizochaguliwa ni Amperra Charging Company (Namibia), Anatsor Ltd na D-Olivette Labs (Nigeria), Mindora Corporation (Zimbabwe), MVUTU (Jamhuri ya Kongo), QualiKeeper Investments Ltd (Zambia), SafeSip (Tanzania), Sesi Technologies Ltd (Ghana), TWave Ltd (Uganda) pamoja na Zerobionic (Kenya).
Akizungumzia mpango huo, Rais wa Mashariki ya Kati na Afrika wa Qualcomm, Wassim Chourbaji, alisema ubunifu unaoonyeshwa na kampuni hizo unaashiria ukuaji mkubwa wa mfumo wa teknolojia barani Afrika.
“Teknolojia kama Edge AI na 5G zina uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii ikiwa zitatumika ipasavyo,” alisema.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Arduino, Fabio Violante, alisema vifaa vya kisasa kama Arduino® UNO™ vinawawezesha wabunifu kubadilisha mawazo yao kuwa suluhisho halisi kwa haraka zaidi.
Mbali na hilo, washiriki watapata msaada wa kulinda miliki bunifu zao, ikiwa ni pamoja na usajili wa hataza kwa kushirikiana na kampuni ya Adams & Adams.
Mpango huo pia unashirikisha African Telecommunications Union kwa mwaka wa nne mfululizo, ambapo Katibu Mkuu wake, John Omo, alisema unasaidia wabunifu wa Afrika kutumia teknolojia kutatua changamoto za bara hilo.
Mwisho wa programu, kampuni zitapata fursa ya kupata ufadhili zaidi pamoja na kurejeshewa hadi dola 5,000 kwa gharama za usajili wa miliki bunifu.
Qualcomm ni kampuni ya kimataifa inayojihusisha na ubunifu wa teknolojia za mawasiliano na kompyuta janja, huku Arduino ikiwa ni jukwaa la wazi la vifaa na programu linalowezesha maendeleo ya miradi ya teknolojia duniani.
https://www.qualcomm.com/
