Waziri wa Madini, Anthony Mavunde,akizungumza katika kikao na wadau wa makaa ya mawe kilichofanyika leo Machi 30,2026 jijini Dodoma.
…
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema makaa ya mawe yana nafasi ya kimkakati katika kuharakisha mageuzi ya uchumi wa Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda,akibainisha kuwa rasilimali hiyo si chanzo cha nishati pekee, bali pia ni mhimili muhimu wa kuongeza thamani ya madini na malighafi nyingine za viwandani.
Amesema kupitia matumizi sahihi ya makaa ya mawe, nchi inaweza kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, kuongeza uzalishaji wa ndani na kuimarisha mnyororo wa thamani katika sekta mbalimbali, ikiwemo nishati, viwanda na madini.
Mavunde ameyasema hayo leo Machi 30, 2026,jijini Dodoma katika kikao na wadau wa makaa ya mawe ambapo amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusikiliza na kutatua changamoto za wadau ili kuhakikisha sekta hiyo inakua kwa kasi na ufanisi.
“Makaa ya mawe ni mhimili muhimu katika maendeleo ya viwanda. Tunahitaji kuongeza uzalishaji na kuhakikisha matumizi yake yanaongeza thamani ndani ya nchi,” amesema Mhe. Mavunde.
Katika kikao hicho, Waziri Mavunde amepokea changamoto mbalimbali kutoka kwa wachimbaji na wafanyabiashara, ikiwemo gharama za uzalishaji, usafirishaji na upatikanaji wa masoko. Ameahidi kuwa Serikali itazifanyia kazi ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Aidha, amesisitiza kuwa upangaji wa bei elekezi utafanyika kwa ushirikishwaji wa wadau wote ili kulinda maslahi ya sekta.
Katika kuimarisha uratibu na mshikamano wa sekta, Mhe. Mavunde amewahimiza wadau kuanzisha chama (association) kitakachowaunganisha, ili kurahisisha shughuli zao na kushughulikia changamoto kwa pamoja kwa ufanisi zaidi.
Katika hatua nyingine ya kuimarisha viwanda vya ndani, Waziri Mavunde amesema kuwa Kampuni ya A1 Steels Tanzania Ltd imepanga kujenga kiwanda cha kuzalisha chuma jijini Dodoma. Kiwanda hicho kinatarajiwa kutumia takribani tani 20,000 za makaa ya mawe kwa mwaka, hatua itakayoongeza mahitaji ya rasilimali hiyo na kufungua fursa zaidi kwa wachimbaji wa ndani.
Mradi huo unatarajiwa kuchochea ajira, kuongeza thamani ya madini na kuimarisha mchango wa sekta ya viwanda katika uchumi wa Taifa.
Kwa ujumla, kikao hicho kimeonesha dhamira ya Serikali ya kuifanya sekta ndogo ya makaa ya mawe kuwa injini ya maendeleo ya viwanda nchini, huku ushirikiano kati ya Serikali na wadau ukiendelea kuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya sekta hiyo.
Kwa upande wao, wadau wa makaa ya mawe wameipongeza hatua hiyo ya Serikali ya kuwashirikisha katika majadiliano, wakieleza kuwa imeongeza uwazi na imani katika uendeshaji wa sekta hiyo. Pia wameahidi kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya ndani na kuongeza mapato ya Taifa.