Featured Kitaifa

MONGELLA AAGIZA SENSA KWA WAFANYABIASHARA SOKO KUU MANISPAA YA SHINYANGA

Written by Alex Sonna

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Ndugu John Mongella, ametoa rai kwa mamlaka ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kuhakikisha inafanya sensa ya kina na ya haki kwa wafanyabiashara wa Soko Kuu la Manispaa hiyo, kabla ya zoezi la ugawaji wa vibanda, ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.

Ndugu Mongella ametoa angalizo hilo leo tarehe 02 Februari, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Shinyanga, alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa Soko Kuu la Manispaa ya Shinyanga.

Akizungumza katika eneo la mradi, Mongella amesisitiza kuwa sensa sahihi itasaidia kubaini wafanyabiashara halali, kuhakikisha haki inatendeka, na kuondoa malalamiko ambayo mara nyingi husababisha migogoro kati ya wafanyabiashara na mamlaka za usimamizi wa masoko.

Ameeleza kuwa Serikali ya CCM inalenga kuona miradi ya maendeleo, ikiwemo masoko ya kisasa, inanufaisha wananchi wote kwa usawa na kuimarisha mazingira bora ya biashara. Ziara hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

About the author

Alex Sonna