Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala, amesema kuwa Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya barabara mbalimbali za mkoa wa Mtwara zinazojengwa kwa kiwango cha lami.
Mkuu wa mkoa ameeleza hayo leo tarehe 08 Januari 2026, wakati akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha bodi ya barabara mkoa wa Mtwara, kilichoketi katika ukumbi wa Benki Kuu Tawi la Mtwara.
Kanali sawala amezitaja barabara za Mnivata-Tandahimba,Newala-Masasi na ile ya Mtwara-Mingoyo Masasi yenye urefu wa 201km, kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa uendelezaji wa miundombinu hiyo ya barabara katika mkoa wa Mtwara.
Ametumia nafasi hiyo kutoa maagizo kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha kuwa miradi yote ya barabara inatekelezwa kwa kuzingatia ubora.
Vilevile Kanali Sawala amesisitiza juu ya TANROADS na TARURA kuwasimamia wakandarasi wanaojenga barabara na madaraja mbalimbali, ili kukamilisha miradi kwa wakati.
Aidha mkuu wa mkoa ametoa maelekezo ya kuhakikisha kuwa wananchi wa maeneo yenye miradi ya barabara, wanapewa kipaombele cha ajira na utoaji wa huduma mbalimbali, bila kuathiri ubora wa kazi husika.