Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha sheria Tanzania, Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Jaji Winfrida Korosso akimkabidhi nyaraka Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Zainabu Katimba wakati wa ziara yake na Waziri katika ofisi za Tume hiyo zilizoko katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) leo Novemba 26,2025.
.Na Mwandishi Wetu – Dodoma
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Zuberi Juma Homera ameiomba Tume ya kurekebisha sheria Tanzania kuainisha sheria zote zilizopitwa na wakati ili ziweze kufanyiwa marekebisho na kufanya kazi zaidi na Watanzania.
Dkt. Homera ameyabainisha hayo leo Novemba 26,2025 Jijini Dodoma wakati alipofanya ziara katika ofisi za Tume hiyo zilizoko katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
“Sisi lazima twende na usasa lakini niwaombe sana mpitie kila Wizara kwamba ukienda Wizara ya Elimu sheria ipi kwasasa imepitwa na wakati, Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na hata Wizara yetu hii kama kuna sheria ambazo zinakuwa zimepitwa na wakati basi ni muda wa kuanza mchakato wa kupitia na kuboresha zaidi,”amesema.
Aidha amemuomba Mwenyekiti na Mtendaji wa Tume hiyo kuhakikisha kila kitengo kinakuwa na mpango wa muda mfupi, mrefu pamoja na mahitaji yake ya bajeti kwaajili ya kufanya kazi ya kufa na kupona ili watanzania waweze kupata sheria zenye matokeo chanya kwaajili ya maisha yao.
“Hakuna sheria inayotungwa kwaajili ya kumkandamiza mwananchi wa Tanzania, mimi sidhani kama hiyo sheria ipo na sheria zote zilizopo ni kwamba mtu umevunja sheria fulani lazima ushtakiwe na anayemshtaki maana yake ni mtanzania na akifungwa maana yake anaye nufaika ni yule ambaye amepeleka shitaka, kwahiyo sheria zote zimetengenezwa kwaajili ya watanzania wote bila ubaguzi “amesema.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Zainab Katimba, ameipongeza Tume ya Kurekebisha sheria Tanzania kwa kazi kubwa wanayoifanya hususani katika eneo la utafiti ambao umesaidia kutengeneza miswada ambayo imefanya maboresho ya sheria inayohitajika.
“Jambo lingine ambalo mnafanya vizuri ni kuhakikisha sheria zetu zinaenda na wakati lakini pia sheria zetu zinaeleweka, kwahiyo hili ni suala kubwa ambalo kwa namna moja au nyingine linaimarisha na kuwezesha upatikanaji wa haki,”amesema.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha sheria Tanzania, Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Jaji Winfrida Korosso amemwakikishia Waziri Dkt. Homera kuwa watafanya kazi kwa ushirikiano na wako tayari kutekeleza majukumu ambayo wamepewa.
Mbali na hayo Jaji Winfrida amebainisha kuwa miongoni mwa sheria ambazo zinahitajika kufanyiwa marekebisho ni pamoja na sheria ya ndoa kwani ina changamoto nyingi ambazo zinapaswa kufanyiwa marekebisho.