Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imezindua ugawaji wa vifaa vya mafunzo ya ubunifu, ushonaji, teknolojia ya nguo na umeme kwa Vyuo vya VETA 63 nchini ili kuimarisha utolewaji wa mafunzo ya ufundi stadi na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Uzinduzi huo umefanywa Novemba 26, 2025 katika Chuo cha VETA cha Wilaya ya Chemba na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Ameir amesema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha VETA inapatiwa vifaa vya kisasa na vya kutosha, pamoja na kuajiri wakufunzi wenye ujuzi na mbinu za kufundishia zinazoendana na wakati.
Amesema Uimarishaji na ongezeko la Vyuo vya VETA nchini ni utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2024 (Toleo la 2023) kwa kutoa fursa za mafunzo kwa vijana ili kuandaa nguvukazi yenye ujuzi inayohitajika katika uzalishaji kwenye sekta mbalimbali.
Mhe. Ameir, amesisitiza umuhimu wa VETA kujielekeza katika mafunzo yanayochochea matumizi ya TEHAMA, Akili Unde na roboti, ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika uchumi wa kidijitali.
kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa vifaa vilivyogawiwa ni msingi mzuri wa mafunzo kwa kuwaandaa wanachuo wawe na uwezo wa kutenda kwa vitendo, kufanya kazi kwa pamoja na kujiandaa ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Antony Kassori, amesema vifaa vilivyonunuliwa na Serikali vina thamani ya shilingi bilioni saba na vitasambazwa katika vyuo 63 vya VETA. Ameongeza kuwa kwa sasa VETA ina zaidi ya vyuo 80 vyenye uwezo wa kudahili wanafunzi 120,000 kwa mwaka, huku vyuo vingine 65 vikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi. Vikikamilika, VETA itakuwa na zaidi ya vyuo 145 vyenye uwezo wa kudahili wanafunzi zaidi ya 250,000 kwa mwaka.
Serikali imeweka bayana kuwa nguvukazi yenye ujuzi na ubunifu ndiyo nguzo ya kufanikisha azma ya Tanzania kuwa na uchumi wa kati unaotegemea uzalishaji kwa wingi na teknolojia ya kisasa.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir,akizungumza wakati akizindua ugawaji wa vifaa vya mafunzo ya ubunifu, ushonaji, teknolojia ya nguo na umeme kwa Vyuo vya VETA 63 nchini,hafla iliyofanyika katika Chuo cha VETA cha Wilaya ya Chemba.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo,akizungumza wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa vifaa vya mafunzo ya ubunifu, ushonaji, teknolojia ya nguo na umeme kwa Vyuo vya VETA 63 nchini,hafla iliyofanyika katika Chuo cha VETA cha Wilaya ya Chemba.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Antony Kassori,akizungumza wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa vifaa vya mafunzo ya ubunifu, ushonaji, teknolojia ya nguo na umeme kwa Vyuo vya VETA 63 nchini,hafla iliyofanyika katika Chuo cha VETA cha Wilaya ya Chemba.
