Mkoa wa Morogoro una mtandao wa Barabara wa kilometa 2,071.23, katika mtandao huo, Barabara kuu ni kilometa 849.43 na Barabara za mkoa ni kilometa 1,221.81.Aidha jumla ya Kilomita 510.37 za Barabara kuu ni za kiwango cha lami na kilomita 339.06 ni za changarawe, kwa Barabara za mkoa kilomita 190.32 ni za lami na kilomita 1,031.49 ni za changarawe.
Mkoa wa Morogoro umepokea kiasi cha shilingi bilioni 712 Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuhudumia miradi ya miundombinu ya Barabara Pamoja na madaraja katika mkoa wa Morogoro huku miradi 7 ya Dharula ya Ujenzi wa Madaraja (CERC) inayofadhiliwa na Benki ya Dunia yenye thamani ya Shilingi bilioni 37.840 ikiwa inaendelea kwa kasi kuboresha miundombinu ya barabara zilizoharibiwa na mvua za El-nino pamoja na Kimbunga hidaya
Hayo yamebainishwa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro Mhandisi John Mkumbo ofisini kwake leo tarehe 25 Octoba 2025 wakati akizungumzia kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani ambaye ametoa shilingi bilioni 712 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya Barabara na madaraja.
Mhandisi Mkumbo ameitaja miradi hiyo kuwa ni Pamoja na Ujenzi Daraja la Chakwale katika Barabara ya Iyogwe – Chakwale – Ngiloli unaojengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 6.438, Ujenzi Daraja la Nguyami Barabara ya Iyogwe – Chakwale – Ngiloli kwa gharama ya shilingi Bilioni 7.166, Ujenzi Daraja la Kihonda katika Barabara kuu ya Morogoro – Dodoma kwa gharama ya shilingi bilioni 5.311, Ujenzi Daraja la Bwage katika barabara Mziha – Turiani na Daraja la Mjonga barabara ya Mvomero – Ndole Kibati kwa gharama ya shilingi bilioni 10.038, Ujenzi Daraja la Doma katika Barabara kuu ya Tanzam kwa gharama ya shilingi bilioni 4.146 na Ujenzi Daraja la Ngerengere katika Barabara kuu ya Morogoro – Dodoma kwa gharama ya shilingi Bilioni 4.737
Amesema kuwa serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya Maendeleo ya kimkakati ya Ujenzi wa barabara na madaraja katika Mkoa wa Morogoro yenye thamani ya shilingi bilioni 670.820 ikiwemo Mradi wa ujenzi wa barabara ya Ubena Zomozi – Ngerengere (Kizuka Army Camp) yenye urefu wa kilomita 11.6 kwa gharama ya shilingi bilioni 20.540, na Mradi wa Ujenzi wa barabara ya Bigwa – Kisaki (sehemu ya Bigwa –Mvuha yenye urefu wa kilomita 78 kwa gharama ya shilingi bilioni 132.015
Mhandiisi Mkumbo ameitaja miradi mingine kuwa ni ujenzi wa barabara ya Ifakara – Kihansi – Mlimba – Taweta – Madeke, Sehemu ya Ifakara – Mbingu yenye urefu wa kilomita 62.5 kwa gharama ya shilingi bilioni 97.178, Mradi wa ujenzi wa barabara ya Ifakara – Kihansi, Sehemu ya Mbingu – Chita JKT kilomita 37.5 kwa gharama ya shilingi bilioni 70.824, Ujenzi wa barabara zinazo elekea katika stesheni za reli ya SGR: (Kihonda kilomita 10 na Rudewa – kilosa kilomita 3) kwa gharama ya shilingi bilioni 27.016 na ujenzi wa barabara kuu ya Ifakara – Lupiro – Malinyi – Londo – Lumecha/Songwe (Forest – Londo -Kitanda); Sehemu ya 1: Ifakara – Lupiro – Malinyi (kilomita 112) kwa gharama ya shilingi bilioni 323.246
Katika mkoa wa Morogoro serikali imekalisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ya kimkakati ya ujenzi wa barabara na madaraja yenye thamani ya shilingi bilioni 205.873, miradi hiyo ni Ujenzi wa Barabara ya Mikumi – Kidatu – Ifakara (Sehemu ya Kidatu – Ifakara, (Kilomita 66.9) kwa kiwango cha Lami pamoja na daraja la Ruaha Mkuu (Mita 133) kwa gharama ya shilingi Bilioni 164.756 na Ujenzi wa Barabara ya Dumila – Kilosa – Mikumi (Kilomita 142) Kwa Kiwango cha Lami, Sehemu ya Rudewa – Kilosa, Kilomita 24 pamoja na ujenzi wa Madaraja matatu ya Kobe (Mita 16), Wailonga (Wailonga mita 20) na Mazinyungu (Mita 20) kwa gharama ya shilingi bilioni 41.116
Mhandisi Mkumbo amebainisha kuwa TANROADS mkoa wa Morogoro inaendelea na hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi Sita (6) ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara zenye thamani ya Shilingi bilioni 3.602 ikiwemo barabara ya Msamvu (Round About) – Morogoro mjini – Bigwa JCT, barabara ya Kizuka Army Camp – Ngerengere – Ngerengere SGR Station Pamoja na Daraja la Ngerengere, Barabara ya Ubenazomozi (Ngerengere SGR station Jct) – Mvuha – Kisaki – Mtemere JCt (159km) Access road kwenda Julius Nyerere Hydropower Project, barabara ya Gairo – Nongwe, kilomita 54, barabara ya Miyombo – Lumuma – Kidete, kilomita 72, Daraja Mkondoa katika barabara ya Dumila – Kilosa – Mikumi na Barabara ya kutoka ya kutoka Geti SUA – Kupitia Mzinga hadi Mzumbe yenye urefu wa kilomita 13 pamoja na madaraja ya Mzinga na Kauzeni.
Aidha Mhandisi Mkumbo ameleza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 22.734 kwa ajili ya kazi za matengenezo ya barabara na madaraja ambapo kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 3.390 ni kwa ajili ya matengenezo ya kawaida ya barabara kuu za lami, bilioni 1.285 ni kwa ajili ya matengenezo ya kawaida ya barabara kuu za Changarawe, bilioni 7.100 ni kwa ajili ya Matengenezo ya Muda maalum Barabara Kuu za lami, bilioni 1.000 ni kwa ajili ya Matengenezo ya Muda maalum Barabara Kuu za Changarawe, milioni 645.373 ni kwa ajili Matengenezo ya kawaida Barabara za Mkoa za lami za Mkoa, bilioni 4.656 ni kwa ajili Matengenezo ya kawaida Barabara za Mkoa za Changarawe, bilioni 1.677 ni kwa ajili ya Matengenezo ya Muda maalum Barabara za Mkoa za Changarawe, milioni 6.000 ni kwa ajili ya Matengenezo ya maeneo korofi, bilioni 1.320 ni kwa ajili ya Matengenezo makubwa ya madaraja (Bridge Major Repair) na bilioni 1.654 ni kwa ajili ya Matengenezo ya kawaida ya Madaraja.