Mkurugenzi wa WiLDAF, Wakili Anna Kulaya
DAR ES SALAAM, Oktoba 23, 2025
Chama cha Wanawake Wanaharakati wa Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF Tanzania) kimetoa wito kwa taasisi zote za serikali, vyama vya siasa, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na asasi za kiraia kuhakikisha wanawake wanalindwa dhidi ya aina zote za ukatili katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumza Oktoba 23, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa Warsha ya Jinsia, Usalama wa Uchaguzi na Haki, Mkurugenzi wa WiLDAF, Wakili Anna Kulaya, amesema ni muhimu mageuzi ya kisheria yaliyofanyika hivi karibuni kutafsiriwa kuwa vitendo halisi vinavyolinda na kukuza ushiriki wa wanawake katika siasa na uchaguzi.
Wakili Kulaya amesisitiza kuwa wanawake wanakumbana na changamoto nyingi katika mchakato wa uchaguzi, zikiwemo vitisho, unyanyasaji, ukatili wa kimtandao, pamoja na rushwa ya ngono. Aliongeza kuwa changamoto hizi huwafanya wanawake wengi kuogopa kujitokeza kushiriki kikamilifu katika nafasi za uongozi na siasa.
“Wanawake kama wapiga kura, wagombea, wanaharakati na hata watoa huduma katika kampeni hukutana na vitisho na udhalilishaji. Rushwa ya ngono imekuwa ikiwadhalilisha kimya kimya lakini kwa maumivu makubwa,” amesema Kulaya.
“Licha ya hayo, wanawake wameendelea kuwa nguzo muhimu ya amani, wanaopunguza mifarakano na misuguano wakati wa uchaguzi. Usawa wa kijinsia si zawadi ni kipimo cha haki. Mwanamke anapaswa kuhakikishiwa usalama kabla, wakati na baada ya uchaguzi,” ameongeza.
WiLDAF imesisitiza umuhimu wa taasisi za kutetea haki za binadamu, wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushirikiana kwa karibu na viongozi wa dini na vyombo vya habari kufuatilia na kuripoti matukio yote ya ukatili wa kijinsia na rushwa ya ngono katika kipindi cha uchaguzi.
Warsha hiyo ililenga kujadili “Jinsia, Usalama wa Uchaguzi na Haki: Kutafsiri Mageuzi ya Kisheria ya Hivi Karibuni kuwa Njia Mahususi za Kulinda na Kukuza Ushiriki wa Wanawake katika Michakato ya Uchaguzi kupitia Ushirikiano wa Taasisi za Serikali, Mamlaka za Uchaguzi, Vyama vya Siasa, Vyombo vya Ulinzi na Usalama, pamoja na Asasi za Kiraia.”















