Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amemuagiza mtumiaji wa mitandao ya kijamii anayefahamika kama Uncle T kufika mbele ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) @basata.tanzania ili kujieleza kufuatia tuhuma mbalimbali kutoka kwa jamii zinazodai kuwa anavunja maadili.
Waziri Dkt. Gwajima ametoa agizo hilo tarehe 4 Oktoba 2025 kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram @gwajimad ambapo amesema wanajamii wa mtandaoni, wamekuwa wakimtumia hoja nyingi kuhusu shughuli za Uncle T huku madai ya wanajamii ni kwamba maudhui yake hayana maadili, yanaharibu vizazi, na kwamba mara nyingi husemekana akemei vitendo hivyo, na kusema kuwa jambo hilo ni muhimu kushughulikiwa.
Aidha, Waziri Gwajima amesema amepitia ukurasa wa Instagram wa @ankot_1 na kujionea machapisho mbalimbali ikiwemo matangazo yanayomwonesha akivaa nguo za kike licha ya yeye kuwa mwanaume.
Amefafanua kuwa suala hilo linapaswa kupata mwongozo kutoka Wizara yenye dhamana ya Utamaduni na Sanaa kwa kuwa maadili ni zao la mila na tamaduni, na Wizara hiyo ndiyo yenye vyombo vya kisheria vinavyosimamia wasanii, filamu na kazi za sanaa kwa ujumla.
Aidha, ameeleza kuwa iwapo Anko T atabainika kuwa na hoja za kujibu, hatua zaidi zinaweza kuchukuliwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kudhibiti machapisho yake, Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kudhibiti biashara zake, Wizara ya Mambo ya Ndani kuchunguza tuhuma dhidi yake, na hatimaye Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Mahakama kwa ajili ya kutoa uamuzi wa mwisho.
Waziri Dkt. Gwajima amehitimisha kwa kueleza kuwa lengo lake ni kutoa mwelekeo wa namna ya kushughulikia malalamiko mbalimbali yanayotolewa na wananchi ili jamii ielewe kuwa si kila hoja inahusu Wizara ya Maendeleo ya Jamii pekee.
Ameahidi kuendelea kutoa elimu juu ya taratibu za kisheria na kiutawala zinazopaswa kufuatwa, ili wananchi waweze kushiriki ipasavyo katika ujenzi wa jamii imara inayozingatia sheria, kanuni na miongozo ya nchi.