Featured Kitaifa

REA YAANZA UHAMASISHAJI KWA WANANCHI KUJIUNGA NA HUDUMA YA UMEME KWENYE VITONGOJI MKOANI SIMIYU

Written by Alex Sonna

Timu ya wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na timu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) tarehe 03 Oktoba, 2025 wameanza zoezi la uhamasishaji kwa Wananchi ili wajiunge na huduma ya umeme kwenye vitongoji mbalimbali vya mkoa wa Simiyu.

Akizungumza na Wanahabari, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka REA, Bi. Jaina Msuya amesema lengo la uhamasishaji huo ni kuongeza hamasa ya kujiunga na huduma ya umeme pamoja na kuongeza uelewa wa faida za matumizi ya nishati ya umeme ili Wananchi wa vijijini wabadili maisha yao kiuchumi na kijamii katika vitongoji vyao.

“Kujiunga na huduma ya umeme wakati mkandarasi akiwa yupo kwenye eneo la Mradi, ni nafuu kwa kuwa Mwananchi atalipia shilingi 27,000 kama gharama ya kujiunga na huduma hiyo ingawa kuna gharama ya kufanya ‘wiring’ na kama Mwananchi atakuwa hana fedha ya kufanya hivyo basi anaweza kununua kifaa maalum kinachitwa *Umeme Tayari* (UMETA) kwa gharama ya shilingi 36,000 tu,” amesema Bi. Jaina.

Kwa upande wake Mhandisi wa Miradi ya Umeme Vijijini mkoani Simiyu, Deusdedit Msanze amesema, uhamasishaji ni muhimu kwa sababu unawakumbusha Wananchi kujiunga na huduma ya umeme ndani ya muda mkandarasi anapokuwa bado yupo kwenye maeneo ya Miradi na kuchelewa kujiunga kunaongeza gharama kwa Wananchi.

Akiwahamasisha Wananchi wa Kitongoji cha Mwamahe, kijiji cha Ikinabushu, kilichopo katika Halmashauri ya wilaya ya Bariadi ambapo mkandarasi, kampuni ya Jiangsu Etern Co., Ltd kutoka China amashakamilisha ujenzi wa miundombinu na Mradi unataji kufungwa tarehe 15 Novemba, 2025 ambapo katika Wananchi 43 wanaostahili kujiunga na huduma ya umeme ni Wananchi saba (7) tu ndiyo waliojiunga na huduma hiyo.

Baada ya uhamasishaji huo Wananchi 20 walijaza fomu ya maombi ya kujiunga na huduma ya umeme ambapo zoezi hilo liliongozwa na Afisa Uhusiano na Wateja kutoka TANESCO mkoa wa Simiyu, Bwana Amon Bidebuye.

Bwana Amon amesema kila Mwananchi mwenye sifa ya kujiunga na huduma ya umeme anaweza kujaza fomu ya maombi kupitia simu ya aina yoyote (Simu Janja au Kiswaswadu) ili kuomba kuunganishwa na huduma ya umeme kwa kupiga *152*00# na baada ya hapo wanatakiwa wafuate maelekezo ambayo ni rahisi.

“Nitoe wito kwa Wananchi, ukitaka kuomba kujiunga na huduma ya umeme, haulazimiki kwenda ofisi ya TANESCO wilayani au mkoani, unaweza kuomba kujiunga kwa kutumia simu yako ya kiganjani na utatakiwa uwe na namba ya NIDA au na Kitambulisho cha NIDA.” amesisitiza Bwana Amon.

Zoezi la uhamaishaji linaendelea katika wilaya ya Itilima na Meatu na Maswa mkoani humo kwa kupitia mikutano kwa Wananchi pamoja na uhamasishaji wa nyumba kwa nyumba.

About the author

Alex Sonna