Featured Kitaifa

WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YATOA VIFAA VYA TEHAMA VYENYE THAMANI YA MILIONI 363

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

Wizara ya Katiba na Sheria imelikabidhi Jeshi la Magereza Vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya shillingi 363, 593, 344.54 kwa lengo la kusaidia utoaji wa huduma za mahakama kwa njia ya mtandao.

Akikabidhi vifaa hivyo leo Juni 19, 2025 katika Ofisi za Wizara Mtumba jijini Dodoma, kwa niaba ya Katibu Mkuu Eliakim Maswi, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Franklin Rwezimula alisema kuwa vifaa hivi vitasaidia uendeshwaji wa mahakama mtandao ambapo mashauri ya kesi yatakuwa yanaendeshwa pasipokuwa na ulazima wa wafungwa kufikishwa katika eneo la mahakama.

“Kwa kutumia vifaa hivi kesi za rufaa na nyingine zitakuwa zinasikilizwa bila wafungwa kufika mahakamani” amesema Dkt. Rwezimula.

Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Kamishina Generali wa Jeshi la Magereza  (CGP) Jeremiah Yoram Katungu, Kamishina wa Sheria na uendeshaji wa Magereza,Nicodemus Tenga amesema kuwa vifaa hivi vinakwenda kutatua changamoto mbalimbali hivyo kuongeza wigo wa utoaji haki.

“Tumepokea seti 30 za vifaa vya TEHAMA ambavyo vitatuongezea wigo wa utoaji haki, tulikua na jumla ya Magereza 66 zenye vifaa hivi kati ya 129, ambapo Magereza 63 hazikua na huduma ya mahakama mtandao, lakini kwa seti hizi 30 jumla ya mahakama 93 zinakwenda kutoa huduma kwa njia ya mtandao hivyo kuongeza wigo wa utoaji huduma za mahakama” amesema.

“Vifaa hivi vitaondoa changamoto mbalimbali zikiwemo gharama za kuwasafirisha wafungwa kutoka Magereza kwenda mahakamani, changamoto za kiusalama wakati wa kuwasafirisha wafungwa hawa pamoja na kusaidia kutoa huduma katika maeneo ambayo hayana mahakama” ameongeza.

Kwa upande wake Gabriel Omar Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA, Wizara ya Katiba na Sheria alisema kuwa katika seti 30 zilizotolewa kila seti ina Televisheni moja ya inchi 65 kwa ajili ya kuwezesha mkutano mtandao kufanyika, komputa mpakato moja, Kamera moja, mashine moja kwa ajili ya kuchapisha majalada, UPS kwa ajili ya kutunza umeme pale unapokatika pamoja na vifaa vya intaneti.

“Vifaa hivi ni kwa ajili ya kusapoti dhana ya mahakama mtandao na vyote vinafanya kazi kwa pamoja, tukiwa na seti hii moja tunawezesha mkutano mtandao ambapo mahabusu wanaweza kusikiliza kesi zao bila wao kufika katika eneo la mahakama” amesema Omar.

About the author

mzalendo