Na.Alex Sonna-DODOMA
MBUNGE wa Mbulu Vijijini (CCM) Mhe.Flatei Massay amehoji kwa nini Serikali haiwaajiri wahitimu wenye Diploma kuwa Watendaji wa Vijiji.
Akiuliza swali leo Mei 22,2025 bungeni Dodoma Mbunge huyo amehoji kwa nini Serikali haiwaajiri wahitimu wenye Diploma kuwa Watendaji wa Vijiji.
Akijibu,Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Festo Dugange amesema ajira za Watendaji wa Vijiji katika utumishi wa umma hufanyika kwa kuzingatia sifa zilizoainishwa katika Muundo wa Utumishi wa Kada za Watendaji wa Vijiji/Mitaa uliotolewa na Serikali kupitia Waraka wa Maendeleo ya Utumishi Na.1 wa Mwaka 2013.
Amesema muundo huo umeainisha Watendaji wa Vijiji/Mtaa wanaoajiriwa katika utumishi wa Umma wanatakiwa kuwa na kiwango cha elimu ya kidato cha Nne (IV) au Sita (VI) waliohitimu mafunzo ya Astashahada (Certificate) katika moja ya fani mbalimbali.
Amezitaja fani hizo ni utawala, sheria, elimu ya jamii, usimamizi wa fedha, maendeleo ya jamii, na sayansi ya sanaa kutoka Chuo cha Serkali za Mitaa (Hombolo) au Chuo chochote kinachotambuliwa na Serikali.
Alisema kutokana na masharti hayo, wahitimu wa mafunzo ya Stashahada (Diploma) katika fani tajwa hawawezi kuajiriwa kwenye Utumishi wa Umma katika nafasi ya Mtendaji wa Kijiji/Mtaa kwa kuwa sifa hiyo haijatajwa katika Muundo husika.
Hata hivyo, wahitimu wenye sifa hiyo wanaweza kuajiriwa katika Utumishi wa Umma katika Kada nyingine zinazotaja sifa hiyo kama sifa ya kuajiriwa.