Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo (kulia) akimkabidhi Tuzo Mkuu wa Kitengo cha Uthibiti Ubora wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof. Atanasia Matemu wakati wa hafla ya utoaji tuzo katika Siku ya Miliki Ubunifu Duniani Mei 21,2025 katika Hoteli ya Johari Rotana Jijini Darces Salaam.
……
Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) imepata heshima kubwa baada ya kutunukiwa tuzo ya kuwa taasisi iliyosajili hakimiliki, iliyotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Miliki Ubunifu Duniani, iliyofanyika Mei 21,2025 katika Hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.
Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu:
“Ulinzi na Matumizi Sahihi ya Miliki Bunifu kwa Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi”, ikisisitiza umuhimu wa kulinda ubunifu na kuutumia kama nyenzo ya kuleta maendeleo endelevu katika jamii.
Akikabidhi tuzo hiyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, ameipongeza NM-AIST kwa kuongoza katika kulinda bunifu na matokeo ya tafiti yanayozalishwa na taasisi hiyo ambapo alieleza kuwa usajili wa hakimiliki ni nguzo muhimu katika kukuza viwanda vya ndani na kuchochea uchumi wa ubunifu.
Akipokea tuzo hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Uthibiti Ubora Prof. Athanasia Matemu kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Taasisi, Prof. Maulilio Kipanyula, ameeleza kuwa tuzo hiyo ni matokeo ya juhudi kubwa zinazofanywa na watafiti, wanafunzi na watendaji wa NM-AIST katika kuhakikisha tafiti zinazofanywa hazibaki katika makaratasi, bali zinapata ulinzi na fursa ya kutumika kwa manufaa ya jamii.
“Hadi sasa NM-AIST imesajili hakimiliki 22, jambo linaloifanya kuwa taasisi ya elimu ya juu inayoongoza kwa usajili wa ubunifu” ameeleza Prof. Matemu.
NM-AIST imekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza ubunifu na ujasiriamali kwa vitendo, kwa kushirikiana na sekta binafsi, taasisi za serikali na mashirika ya kimataifa, ambapo taasisi imekuwa ikiibua suluhisho kwa changamoto mbalimbali katika sekta za kilimo, afya, mazingira na viwanda.
Mbali na utafiti, taasisi hii pia inaweka msisitizo mkubwa kwenye matumizi ya teknolojia kama kichocheo cha maendeleo ya Afrika kupitia programu zake za uzamili, uzamivu na mafunzo endelevu ya uzamivu, aidha, NM-AIST inawaandaa wataalamu na wabunifu ambao si tu watabeba taaluma bali pia watatatua changamoto halisi za jamii na viwanda.
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo (kulia) akimkabidhi Tuzo Mkuu wa Kitengo cha Uthibiti Ubora wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof. Atanasia Matemu wakati wa hafla ya utoaji tuzo katika Siku ya Miliki Ubunifu Duniani Mei 21,2025 katika Hoteli ya Johari Rotana Jijini Darces Salaam.
Tuzo iliyotolewa kwa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela kama Taasisi iliyongoza katika kusajili Hakimiliki za Bunifu Tanzania.