Featured Kitaifa

WAZIRI KIJAJI ATAJA MAFANIKIO MIAKA MINNE YA RAIS SAMIA

Written by mzalendoeditor
WAZIRI  wa Mifugo na Uvuvi Dkt.Ashatu Kijaji,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Mei 6,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
……
WAZIRI  wa Mifugo na Uvuvi Dkt. Ashatu Kijaji amesema katika katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Wizara hiyo imeendelea kuimarisha biashara ya nyama kwenda nje ya nchi, ambapo, mauzo yameongezeka kutoka tani 1,774 zenye thamani ya shilingi bilioni 9.8 kwa mwaka 2020/2021 na kufikia tani 13,745.38, zenye thamani ya shilingi  Bilioni 147.1 kwa mwaka 2024/2025.
Dkt. Kijaji ameyabainisha hayo leo Mei 6,2025 Jijini Dodoma wakati aikizungumza na waandishi wa habari kuhusu  mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi hicho chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuanzia Machi 2021 hadi Aprili, 2025.
“Ongezeko hili linatokana na jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuongeza ushirikiano na fursa za kibiashara nje ya nchi na hivyo, kuongezeka kwa masoko ya nyama hadi kufikia nchi 12 ambazo ni Bahrain, Comoro, Hong Kong, Jordan, Kenya, Kuwait, Oman, Qatar, Rwanda, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Vietnam,”amesema.
Sambamba na hayo Dkt. Kijaji ameongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na Taasisi za Fedha, Sekta Binafsi na Wadau wa Maendeleo imewezesha kutolewa kwa mikopo kwa wafugaji na vikundi vya wafugaji wadogowadogo, ambapo mikopo hiyo ilitolewa kupitia Benki ya TADB imeongezeka kufikia shilingi bilioni 267.09 hadi kufikia Machi, 2025 kutoka shilingi bilioni 2.19 zilizotolewa mwaka 2021.
“Mikopo hii imeendelea kuongezeka kwa ajili ya kuwawezesha wafugaji wadogo pamoja na vikundi vya wafugaji katika ununuzi wa ng’ombe wa maziwa (mitamba), unenepeshaji wa mifugo, ununuzi wa kuku wa mayai na nyama na uchakataji wa maziwa. Aidha, idadi ya wanufaika wa mikopo hiyo mpaka sasa imefikia wanufaika 22,163,”ameongeza.
Aidha, ameongeza kuwa kwasasa Sekta ya Uvuvi ni miongoni mwa Sekta za uzalishaji ambayo inatoa ajira za moja kwa moja kwa wavuvi 201,661 ambapo ukuaji wa Sekta ya hiyo ni asilimia 1.4 na kuchangia Pato la Taifa kwa asilimia 1.7 katika mwaka 2023.
Hali ya uzalishaji wa mazao ya uvuvi umeongezeka kutoka tani 477,018.84, zenye thamani ya shilingi Bilioni 2.7 katika mwaka 2021, hadi kufikia tani 522,788.33, zenye thamani ya shilingi Bilioni 4.3 katika mwaka 2024.
“Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2024, jumla ya tani 1,951,296.33 za mazao ya uvuvi, zenye thamani ya shilingi 13,647,504,498.08, zilizalishwa kutoka katika maji ya asili,”amesema.
Pia, ameongeza kuwa Serikali imeendelea na ujenzi wa miundombinu ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji ikiwa ni pamoja na kukamilisha na kuendelea na ujenzi wa Masoko saba (7) ya Samaki ya Tunduma – Songwe, Manda – Ludewa, Zingibari – Mkinga, Kasanga – Kalambo, Masuche – Momba, Kyamkwikwi – Muleba na Mbamba bay – Ruvuma.

About the author

mzalendoeditor