Featured Kitaifa

NDOA YA EVA: KUPITIA MATESO NA ULEMAVU, HATIMAYE KIFO

Written by mzalendoeditor

 

Huzuni kubwa ilitanda miongoni mwa watu tuliokuwepo wakati mwanamke mmoja aliposhuka kwenye gari kwa tabu huku akiwa na magongo.
 
Binafsi nilikuwa nimevunjika mguu na nilikuwa siko sawa sana kisaikolojia lakini nilipomwona mwenzangu, ghafla nilihisi nimepona. Kwa kweli mtu hakuhitaji kuuliza kujua kuwa mwanamke huyo alikuwa amepata ajali kubwa sana katika maisha yake.
 
Nilimsaidia kushuka na baadae nikaita waandishi wenzangu na tukaa kumhoji kwani tulijuzwa kwamba alikuwa na madhira makubwa ambayo alikuwa ameyapata. Tukio hili lilitokea miaka 15 iliyopita lakini bado ninakumbuka uso wa mwanamke huyo ambaye baadae nilikuja kujua kuwa anaitwa Eva.
 
Swali langu la kwanza nililomuuliza Eva ilikuwa kuhusiana na aina ya ajali aliyopata kwani niliamini lazima alipata ajali kubwa sana. Alisita kwanza kuniambia na baadae akanijuza kwamba alikuwa ameolewa na alikuwa na watoto watatu na ndipo akaanza kunisimulia.
 
“ Ndoa yangu imekuwa na mateso sana. Nimekuwa nikivumilia vipigo ambapo mume wangu alifikia hatua ya kunichoma na pasi hapa kwenye ziwa lakini nimekuwa navumilia kwa ajili ya Watoto lakini kwa sasa nimechoka,” alisema Eva huku akinionyesha kidonda kikubwa kwenye ziwa lake.
 
Niliendelea kumdodosa zaidi anijuze ajali iliyomsababishia yeye kutembea na magongo na ndipo aliponijuza kwamba kulitokea kutoelewana kati yao na katika mabishano mume wake alimsukuma kutoka ghorofa ya kwanza ya nyumba yao hadi chini ambapo alivunjika uti wa mgongo.
 
“ Nililazwa hospitalini ambapo madaktari wameniambia kwamba maisha yangu yote itanibidi kutembelea magongo kwani niliumia vibaya,” alisema Eva huku akifuta machozi.
 
Ukimya mkubwa ulitawala mahali pale na ilituchukua muda kuendelea na mahojiano hayo. Baadae nilimtafuta mume wake ambae alikuwa mkali ambapo pia alitoa vitisho.
 
Juhudi zilifanyika ambapo mume wake Eva alikamatwa huku wanasheria wakihangaika kumpa msaada wa kisheria.
 
Niliendelea kufuatilia hali ya Eva kwa karibu lakini wiki mbili baadae nilipatwa na mshtuko mkubwa Eva aliponiambia kwamba ameamua kufuta mashtaka na kurudi kwa mume wake.
 
Nilitumia muda mrefu sana kumshauri na kumuasa kuwa kama mwandishi nilihisi kwamba simulizi yangu nitakayoandika baada ya hapo huenda isiwe nzuri sana kwani nilihisi kabisa
 
atakumbwa na jambo baya kwani sikuamini kwamba mume wake atakuwa amebadilika hata kidogo.
 
Ni miaka 15 imepita toka nifanye mahojiano na Eva. Mapema mwaka huu tulikuwa na kikao kuongelea masuala ya ukatili nikatoa mfano wa Eva namna alivyorudi licha ya kupewa ulemavu huku nikisema natamani kujua anaendeleaje. Mkuu wangu wa kazi ambae tulishirikiana nae kufanya usaidizi kwa Eva aliniita pembeni na kunijuza kuwa Eva alifariki dunia wiki moja tu baada ya kurudi nyumbani kwake kwenye ndoa. Nilipata maumivu makubwa na sijui nini kilimuua.
 
Zipo simulizi nyingi sana zinazoendana na Eva. Kwa sasa, vitendo vya mauaji ya wenza vimeshika kasi huki vingi vikichangiwa na watu kujaribu kuvumilia kwa matumaini kuwa mwenza huyo atabadilika.
 
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) pamoja na mashirika mengine ya kifeminia yamekuwa yakishauri umuhimu wa kujenga nyumba salama ambapo wahanga wa ukatili watakaa na kupata misaada yote ikiwemo ya kiafya, unasihi na matibabu. Uwepo wa nyumba hizo unaweza kusaidia wahanga wa ukatili lau kuwa na muda wa kutafakari wakati wakipanga kusonga mbele. Upo pia umuhimu wa kuwekeza kwenye afya ya akili kwani ni dhahiri kwamba ni ngumu kwa mtu mwenye akili timamu kumuua mwenza na kuendelea na maisha kama hakuna kitu kinachoendelea.
 
Ni vema pia wazazi tukawafundisha watoto wetu wote wa kiume na kike kwamba ni afadhari waondoke na hata kurudi nyumbani iwapo mahusiano au ndoa zina vitendo vya ukatili kuliko kuvumilia na kurudi kwenye jeneza. Nyakati zimebadilika sana lakini ipo haja ya viongozi wa dini, wa mila na wadau wote kuendelea kufanya kazi ya kutokomeza ukatili kwani hali inatisha.
 
Mungu aziweke mahali pema peponi roho za wahanga wa ukatili kama Eva na wengineo.

About the author

mzalendoeditor