Featured Kitaifa

TANZANIA MWENYEJI MKUTANO WA FORODHA AFRIKA MASHARIKI NA KATI – FIATA RAME 2025

Written by mzalendoeditor

Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Shirikisho la vyama vya mawakala wa ushuru wa forodha kwa upande wa Afrika Mashariki na kati (FIATA-RAME) unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Akiongea na waandishi wa habari tarehe 8 Machi, 2025 Kwenye Hotel ya Golden Tulip iliyopo Unguja,Zanzibar Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema mkutano huo utafanyika kwenye hotel hiyo kuanzia tarehe 30 April mpaka Mei mosi mwaka huu.

Akisistiza juu ya umuhimu wa mkutano huo wa kila mwaka, Profesa Mbarawa amesema mkutano huo utawaleta pamoja wadau wakuu na wataalamu wa sekta ya usafirishaji ,uchukuzi na sekta mtambuka zaidi ya 500 ili kujadili fursa, changamoto, na ushirikiano katika sekta hiyo.

Amesema Kaulimbiu ya mkutano huu ni “Ushirikiano katika Uchumi wa Buluu: Kubadilisha Sekta ya Usafirishaji na Uchukuzi kwa Maendeleo Endelevu” ambayo inaendana na jitihada za Serikali ya Tanzania kuboresha miundombinu ya uchukuzi chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi.

Pia Profesa Mbarawa amewaambia wanahabari kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ndiye anayetarajiwa kuzindua rasmi mkutano huo Aprili 30.

Aidha Profesa Mbarawa amewataka wadau wa sekta ya uchukuzi nchini Tanzania, Afrika Mashariki, na kwingineko kutumia jukwaa hili la kimataifa kuunda ushirikiano na kupata maarifa kuhusu mustakabali wa sekta ya usafirishaji na uchukuzi na kuwataka wadhamini kuchangamkia fursa

Awali Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi, Zanzibar anayeshughulikia masuala ya ujenzi na uchukuzi Mhe Makame Machano amevipongeza vyama vya ushuru vya Bara na Zanzibar kwa jitihada na mafanikio za kuiletea fursa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu mkubwa

Akizungumzia Mkutano huo Rais wa Chama cha Mawakala wa Ushuru na Forodha Tanzania Bw Edward Urio ametoa shukran za dhati kwa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano huu wa kimataifa kwa upande huu wa Afika ya mashariki na kati wa RAME na kuongeza kuwa mkutano huu ni matokeo ya jitihada za TAFFA na ZFB tokea April, 2024.





About the author

mzalendoeditor