Featured Kitaifa

MABINTI WA VYUO VIKUU WASEMA NI RAIS SAMIA MITANO TENA

Written by mzalendoeditor

Kongamano kubwa la ‘Binti wa Leo, Samia wa Kesho’ linatarajiwa kufanyika Jumamosi Machi 08, 2025, katika ukumbi wa Bwalo la Jeshi, Kona ya Nyegezi jijini Mwanza, likilenga kuhamasisha mabinti wa vyuo na vyuo vikuu kutimiza malengo yao kwa kutumia mifano ya mafanikio ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 Kongamano hili ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, na linajumuisha mabinti kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza, Verynancy Mrema, Makamu Mwenyekiti wa kampeni ya ‘Mama Asemewe’, amesema kuwa kongamano hili ni fursa muhimu ya kujifunza kutoka kwa Rais Samia, ambaye amekuwa kipenzi cha wengi kutokana na juhudi zake za kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu bora na nafasi sawa na watoto wa kiume. 

“Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mfano wa kuigwa kwa wanawake na mabinti nchini Tanzania. Katika kipindi kifupi cha utawala wake, ameleta mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na elimu, afya, na usawa wa kijinsia”,amesema. 

“Mojawapo ya mafanikio yake ni juhudi za kuboresha elimu ya mtoto wa kike, ambapo serikali yake imejenga shule maalum za sekondari za wasichana katika mikoa 26 ya Tanzania. Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa watoto wa kike wanapata fursa bora za elimu, huku akisisitiza kuwa elimu ni ufunguo wa maendeleo ya taifa”,ameongeza.

Amesema pia, Rais Samia ameonesha kuwa wanawake wanaweza kushika nafasi kubwa za uongozi, akichaguliwa kuwa rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania, jambo ambalo limekuwa mfano thabiti wa usawa wa kijinsia. 

“Mafanikio haya ya Rais Samia yanawahamasisha mabinti wengi kujiamini na kufanya bidii katika kutimiza malengo yao, huku wakikumbuka kuwa nafasi ya uongozi inapatikana kwa kujituma na kujitolea”,ameeleza.

Mrema amesisitiza kuwa mabinti wanapaswa kuchukua mifano ya Rais Samia kama chanzo cha motisha na kufanya juhudi kubwa ili kuwa viongozi wa kesho.

Vilevile, Mrema amebainisha kuwa bado kuna changamoto zinazowakabili mabinti vyuoni ikiwemo ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi, magonjwa ya zinaa, ndoa na mimba za mapema kabla ya wakati hivyo wanaomba Rais Dkt. Samia awasaidie kuanzisha taasisi itakayowasaidia mabinti wa vyuo na vyuo vikuu nchini ambapo wamependekeza taasisi hiyo iitiwe ‘Binti wa Leo, Samia wa Kesho Foundation’.

Naye Katibu wa kampeni ya ‘Mama Asemewe’ Mkoa wa Mwanza, Marietha Mtawa amewahimiza mabinti wa vyuo na vyuo vikuu jijini Mwanza kujitokeza kwa wingi kwenye kongamano hilo litakalowasaidia kuhamasisha kupitia mifano ya mafanikio ya Rais Dkt. Samia.
 
Kwa upande wake Katibu Idara ya Vijana na Uhamasishaji kampeni ya Mama Asemewe, Furaha Panja amesema palipo na mafanikio ya mabinti, vijana pia hawakosi hivyo nao wajitokeze kwenye kongamano hilo na kuunga mkono juhudi zake za kuhamasisha mabinti kuwa viongozi wa kesho.

Kongamano hili linatarajiwa kuwa ni jukwaa muhimu la kuhamasisha mabinti wa vyuo na vyuo vikuu kujitahidi kufikia malengo yao, huku wakichukua hatua za kuwa viongozi wa kesho na kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Na George Binagi- GB Pazzo, Mwanza

Makamu Mwenyekiti wa kampeni ya Mama Asemewe, Verynancy Mrema (katikati akizungumzia kongamano la Binti wa Leo, Samia wa Kesho linalotarajiwa kufanyika jijini Mwanza. Kulia ni Katibu wa Idara ya Mabinti na Uwezeshaji wa kampeni ya Mama Asemewe, Benedicta Oshoa na kushoto ni Katibu wa kampeni hiyo Mkoa wa Mwanza, Marietha Mtawa.
Makamu Mwenyekiti wa kampeni ya Mama Asemewe, Verynancy Mrema akizungumza na wanahabari jijini Mwanza kuelekea kongamano la Binti wa Leo, Samia wa Kesho.
Makamu Mwenyekiti wa kampeni ya Mama Asemewe, Verynancy Mrema akizungumza na wanahabari jijini Mwanza kuelekea kongamano la Binti wa Leo, Samia wa Kesho.
Mabinti wa vyuo na vyuo vikuu nchini wakiwa tayari kwa kongamano la Binti wa Leo, Samia wa Kesho.
Mabinti wa vyuo na vyuo vikuu nchini wakiwa tayari kwa kongamano la Binti wa Leo, Samia wa Kesho.
Wanasema, ‘Mama Mitano Tena’.
Wanasema, ‘Mama Mitano Tena’.
Wanasema, ‘Mama Mitano Tena’.
Katibu Idara ya Vijana na Uhamasishaji kampeni ya Mama Asemewe, Furaha Panja akihamasisha vijana jijini Mwanza kushiriki kongamano hilo.

About the author

mzalendoeditor