Na Mwandishi Wetu Gairo, Morogoro
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani Gairo mkoani Morogoro inatekeleza mradi wa ujenzi wa makalavati tisa katika barabara ya Iyogwe – Chogoali yenyewe urefu wa Km 19 itakayowanufaisha wananchi wa wilaya tatu za Mvomero, Kilindi na Gairo.
Ujenzi wa makalavati hayo unaotekelezwa kupitia mradi wa RISE sehemu ya uondoaji wa vikwazo katika barabara unatekelezwa wilayani humo kwa lengo la kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji kwa wananchi hususani wa maeneo ya vijijini.
Meneja wa TARURA wilaya ya Gairo, Mhandisi Simon Masala amesema kuwa mradi huo unalenga kuwasaidia wananchi kuzifikia huduma za kijamii na kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.
Naye, Diwani wa Kata ya Iyogwe Mhe. Clemence Msulwa amesema kuwa ujenzi wa makalavati hayo itawasaidia watu wa upande wa Iyogwe kwenda Masimbani na Chogoali kwa ajili ya shughuli za kilimo.
“Kipindi cha mvua ilikuwa ni shida kwenda kwenye shughuli za kilimo lakini makalavati haya yatatusaidia kwenye uchumi kutoka Wilaya za Mvomero na Kilindi kuja Wilaya ya Gairo, kwa hiyo ni barabara unganishi katika shughuli za kiuchumi kwenye maeneo yetu”, amesema.
Kwa upande wake Mkazi wa Kitongoji cha Ibong’o, Bi. Jeliani Mhadu amesema kuwa kabla ya ujenzi walikuwa wakipata shida hasa maji yakijaa ambapo iliwazuia kuvuka kwenda kuchota maji kwenye kisima ambacho kipo upande wa pili wa mto.
“Wajawazito tulipokuwa tukihitaji huduma ya afya katika zahanati ya Iyogwe tulikuwa hatuwezi kupita kwa sababu maji yamejaa mpaka tupate wafadhili ambao ni wavulana watuvushe ndipo tukapate huduma kwenye zahanati ya Iyogwe lakini sasa tunashukuru tumeondokana na adha ya kutembea kwenye maji”.