Featured Kitaifa

TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA DUNIA WA MASUALA YA MAWASILIANO YA SIMU NCHINI HISPANIA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry William Silaa (Mb) ameshiriki katika Mkutano wa Dunia wa Masuala ya Mawasiliano ya Simu (Mobile World Congress 2025) unaofanyika kuanzia tarehe 03 – 05 Machi, 2025 katika mji wa Barcelona, Hispania.

Katika mkutano huo Waziri Silaa amepata nafasi ya kushiriki katika mijadala kwenye masuala ya Ujumuishaji wa uunganisho wa (Direct to device ;D2D )katika mfumo wa mawasiliano na namna ya kukabiliana na changamoto za masafa; Uboreshaji wa Mifumo ya Usimamizi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (USF) katika nchi za Afrika ambapo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote wa Tanzania (UCSAF) umekuwa mfano kati ya mifuko inayoendeshwa kwa uwazi na mafanikio na mada nyingine ilikuwa ni Uwepo wa Bei nafuu za Masafa zinazochochea Usawa.

Wakati huo huo, Waziri Silaa ameshiriki Mjadala wa Kitaifa (National Dialogue Tanzania: Towards a Fully Digitalized Economy) katika kikao cha pembeni na Kampuni ya Watoa Huduma za Mawasiliano Duniani (GSMA) ambao ni waandaji wakuu wa mkutano wa MWC 2025.

Katika mjadala huo, GSMA iliwasilisha taarifa ya tathmini ya changamoto za Sekta ya Mawasiliano kwenye nchi nne za Afrika ambazo ni Nigeria, Kenya, Ethiopia, Zambia na Afrika Kusini.

Waziri Silaa alitumia mkutano huo kutangaza Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa Tanzania uliozinduliwa 29 Julai 2024 na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kuhamasisha GSMA kuwakaribisha wanachama wake kushiriki utekelezaji wake.

Mkutano wa Dunia wa Masuala ya Mawasiliano ya Simu wa mwaka 2025 unakutanisha watunga sera katika Sekta ya Mawasiliano, Wabunifu mifumo na programu na suluhisho mbalimbali katika teknolojia ya simu, watoa huduma za simu za mkononi, na watafiti.

Vile vile, MWC 2025 ni jukwaa kubwa la makampuni ya teknolojia kuonesha bidhaa mpya tofauti katika simu za mkononi, vifaa vya kuunganishwa na suluhisho mbalimbali za kiteknolojia.

About the author

mzalendoeditor