Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa (Rufaa) Jacobs Mwambegele akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Nyuki Kata ya Lukobe wakati alipokitembelea kituo hicho cha ofisi ya Serikali za Mtaa kukagua zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililoanza leo Machi mosi, 2025 mkoani Morogoro.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa (Rufaa) Jacobs Mwambegele akizungumza na wananchi wakati akifatilia mwenendo wa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililoanza leo Machi mosi, 2025 mkoani Morogoro.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa (Rufaa) Jacobs Mwambegele akiangalia namna mwendesha kifaa cha biometriki akichukua picha ya mwananchi aliyefika kuboresha taarifa zake katika kituo cha Mafiga B kata ya Mafiga mkoani Morogoro leo.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa (Rufaa) Jacobs Mwambegele akimkabidhi Kadi ya Mpiga Kura Ramadhani Waziri ambaye ni mpiga Kura Mpya wa Kata ya Mafiga Mkoani Morogoro.
Ramadhani Waziri ambaye ni Mpiga Kura Mpya wa Kata ya Mafiga Mkoani Morogoro akionesha kadi yake baada ya kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Mpiga Kura mpya Joyce Salehe mkazi wa Kata ya Boma katika Manispaa ya Morogoro akionesha kadi yake.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Rufani, Jacobs Mwambegele akitembelea vituo hii leo akiwa na Afisa Mwandikishaji wa Manispaa ya Morogoro, Ndg. Faraja Maduhu.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Rufani, Jacobs Mwambegele akitembelea vituo hii leo.
Na Mwandishi wetu, Morogoro.
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema
kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa wananchi kujitokeza katika vituo mbalimbali vya
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaofanyika mkoani Morogoro na sehemu ya mkoa wa Tanga kwa siku
saba kuanzia Machi mosi hadi 7, 2025.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,
Jaji Rufani, Jacobs Mwambegele alisema hayo Machi 1, 2025 alipokua akishuhudia
zoezi la uboreshaji wa Daftari wa Kudumu la Wapiga Kura lilivyokuwa
linaendelea kituo cha Mafiga B, Kata ya
Mafiga , Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
“Nimekuja kushuhudia jinsi zoezi hili
linavyoendelea, Saa 2:00 kamili vituo vimefunguliwa na nimefika katika Kituo
cha Mafiga B ambako kituo kilifunguliwa Saa 2 asubuhi na wananchi wengi sana
wamejitokeza katika kuboresha taarifa zao au kujiandikisha kuwa Wapiga
Kura,”alisema Jaji Mwambegele.
Alisema ametembelea vituo vingi na wananchi
wamejitokeza kwa wingi kuboresha taarifa zao au kujiandikisha na alitoa wito
kwa wakazi wa manispaa ya Morogoro na mkoa mzima wa Morogoro kujitokeza kwa
wingi katika zoezi hilo.
“Nawasihi wakazi wa Manispaa ya Morogoro
kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha au kuboresha taarifa zao, nawasihi
wafanye hivyo mapema iwezekanavyo kwani zoezi hili limaenza leo na litachukua
muda wa siku 7 mpaka hapo tarehe
7,2025,”alisema Jaji Mwambegele.
Amesema Wananchi wasisubiri mwisho ndio
wakaja kujiandikisha bali wafanye hivyo mapema na wasubiri tu tarehe ya
Uchaguzi Mwezi Oktoba ili wapige Kura kuwachagua viongozi wanaowataka.
Akizungumzia changamoto iliyobainika na
kufanya watu kukaa muda mrefu vituoni, Jaji Mwambegele alisema wamebaini kuna
watu wamesahau majina yao waliyoyatumia kujiandikisha hapo awali hivyo hutumia
muda mrefu kutafuta katika mfumo.
“Kunachangamoto kidogo imejitokeza katika
kuwatafuta wale waliokuja kuboresha taarifa zao, wengi inachukua muda kumpata
kwa sababu amesahu majina yake, jina la kwanza analiweka la pili au saa
nyingine anakosea ‘speling’ kwa mfano wewe kama unaitwa Zaituni inaandikwa na
‘i’ mwisho au bila ‘i’ sasa unapotamka jina ambalo linatofautiana na lilivyo
katika data base yetu inachukua muda kukupata, alisema.
Amewasihi wananchi wakumbuke majina yao kama
ni Khadija inaanza na K wakumbuke namna hiyo au kama ni Hadija ina anza na H
wakumbuke namna hiyo na kama ni Mohammed
au Muhammed wakumbuke katika
kutamka majina yako vizuri.
Kwa mujibu wa ratiba, kwa sasa Tume imeanza
Uboreshaji wa Daftari wa Kudumu la Wapiga kura mzunguko wa 12 kati ya mizunguko
13 iliyopangwa na Tume kwa mkoa wa Morogoro na Halmashauri Nne za Bumbuli,
Handeni, Mkinga na Pangani zilizopo mkoani Tanga limeanza leo Machi mosi na
litafika tamati Machi 07, 2025 na litadumu kwa siku saba huku vituo
vikifunguliwa Saa 2:00 asubuhi na kufungwa Saa 12:00 jioni.