Featured Kitaifa

TARURA YAKAMILISHA UJENZI WA DARAJA LA MTO IFUME, TANGANYIKA

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Katavi.

Wananchi wa vijiji vya Itunya na Songambele kata ya Kapalamsenga, Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, wameishukuru Serikali kupitia TARURA kwa kuwajengea daraja la kudumu la mto Ifume lenye urefu wa mita 40 linalounganisha vijiji hivyo na maeneo yao ya kilimo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema, hapo awali walikuwa wakipata shida kupita katika eneo hilo kutokana na kukosekana kwa daraja hasa kipindi cha masika hali iliyochangia kuwarudisha nyuma kiuchumi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Itunya, Bw. Michael Lupasha, ameishukuru serikali kwa kuwajengea daraja la mto Ifume kwani wananchi walikuwa wanatumia nauli sh. 15,000/= kusafiri kwenda mjini lakini sasa hivi wanatumia nauli sh. 9000/= na kuzifikia huduma za kijamii kiurahisi.

“Sisi ni wakulima tunazalisha mahindi, maharage, mtama, viazi, mihogo, mpunga lakini pia kuna wachimbaji wadogowadogo wa madini ya dhahabu na shaba, kupitia daraja hili wananchi sasa wanafanya biashara zao kwa uhuru na uchumi wao kukua”, alisema.

Naye, Bi. Caroline Chambala mkazi wa kitongoji cha Milundumo amesema kabla daraja hilo walipata adha kubwa kuvuka mto kipindi cha mvua ambapo watu wengi wamefariki, pia wajawazito walipata shida kwenda kujifungua lakini sasa hivi wanaishukuru serikali wanavuka bila shida yoyote.

Bw. Nobart Ndibasana mkazi wa Milundumo, amesema wakulima walikuwa wanatumia hadi wiki kwenda mashambani wakisuburi maji yapungue ambapo vyakula vilikuwa vinaharibika mashambani, lakini sasa hakuna tena changamoto hiyo baada ya kujengewa daraja la kudumu.

Kwa upande wake, Mhandisi Bonaventura Katambi, msimamizi wa mradi kutoka TARURA wilaya ya Tanganyika, ameishukuru serikali kwa kuwapatia fedha ambazo zimewezesha kuboresha usafiri na kuondoa vikwazo kwa wananchi na kuwawezesha kuendelea na shughuli zao za kijamii na kiuchumi.

Amesema mradi wa RISE sehemu ya uondoaji vikwazo katika barabara wilayani Tanganyika utekelezaji wake umefikia asilimia 80 na kazi wanazozitekeleza ni ujenzi wa daraja la mawe la mto Ifume mita 40, ujenzi wa barabara ya Kapalamsenga-Itunya Km 8.3 pamoja na makalavati.

About the author

mzalendo