Featured Kitaifa

WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA NA TPSF ZAFANYA KIKAO CHA MAJADILIANO

Written by mzalendoeditor

Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara imekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Januari 22,2025 katika ukumbi wa Mikutano wa FCC jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yameongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt.Hashil Abdallah ambapo amesema kuwa mazungumzo hayo ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kukaa,kukutana na kujadili mambo yote yayorahisisha shughuli za ufanyaji biashara nchini.

Aidha Dkt.Abdallah amesema katika majadiliano hayo wamepanga kufanya vikao endelevu na kuadhimia kufanyika kwa mkutano mkubwa wa kiseta MPPD ambapo utakuja kufanya majumuisho yaliojadili katika Mkutano huo.

Vilevile ametoa pongezi kwa Shirikisho hilo kwa kuboresha Sera zao na Muundo unaoendana na falsafa za awamu ya sita na kwa kufanya hivyo Serikali itakuwa bega kwa bega na Shirikisho hilo kwani wamedhihirisha kuwa sekta hiyo inabadilika kulingana na mazingira ya Mifumo ya Biashara.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho hilo Bi.Angelina Ngalula amesema kuna mabadiliko wameyafanya kwenye uendeshaji wa taasisi ili kuweza kutoa mchango mkubwa kwa Serikali katika kuimariaha uchumi wa nchi.

Amesema mabadiliko hayo yamefanywa kwenye nyanja za Teknolojia, masuala ya kidigitali ,wafanyabiashara wadogo,vijana ,afya,elimu na mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na kujumuisha taasisi na Mabaraza ya Wilaya ili kutatua kero na kujenga uelewa wa mipango ya Shirikisho na mifumo.

Vilevile ameishukuru Wizara na Taasisi zake kwa ushirikiano kati yao ambao umeboresha utendaji kazi wa Shirikisho kuliko miaka 4 iliyopita ambayo ilikuwa na malalamiko makubwa hasa kwenye tozo pamoja na kuanza mapema maandalizi ya Maonesho ya OSAKA-EXPO nchini Japani.

About the author

mzalendoeditor