Na Philipo Hassan – Zanzibar
Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Jenerali (Mstaafu) George Waitara, jana Desemba 18, 2024 walitembelea maeneo mbalimbali ya utalii Visiwani Zanzibar kwa lengo la kujifunza utalii wa visiwa, kihistoria na malikale.
Ziara hiyo yenye lengo la kujifunza masuala ya utalii wa kihistoria na malikale pamoja na kujenga mahusiano imefanyika katika Kisiwa cha “Prison Island”, Makumbusho ya Jumba la Kale la Wananchi (na mji mkongwe “Stone town” ambapo wajumbe wa bodi na timu ya Menejimenti ya TANAPA ilipata fursa ya kutembelea maeneo yenye vivutio vinavyofanana na maeneo wanayosimamia ikiwa ni pamoja na Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Kisiwa cha Rubondo na pia vituo vya vya malikale; Caravan Serai – Bagamoyo, Dr Livingstone, Ujiji Kigoma,
Kisiwa cha Prison kimebeba historia ya enzi za ukoloni ambapo kilikuwa ni gereza kwa ajili ya watumwa na kituo cha karantini kwa wagonjwa wa magonjwa ya kuambukiza. Kisiwa hiki ni kivutio cha utalii maarufu kwa historia yake na makazi ya kobe wakubwa wa Aldabra, waliotolewa kama zawadi kutoka visiwa vya Shelisheli mwaka 1919 na Serikali ya Uingereza, iliyokuwa ikitawala wakati huo.
Aidha, Bodi ilitembelea eneo la Stone town, mji wa kihistoria wa Zanzibar, ambao ni kitovu cha urithi wa tamaduni na biashara katika Afrika Mashariki. Mji huu ulijengwa kati ya karne ya 18 na 19, ikiwa kituo cha biashara ya watumwa, viungo (hasa karafuu), na pembe za ndovu. Safari hii iliambatana na matembezi ya miguu katika eneo la kihistoria la Makaburi ya Machifu/Wafalme waliowahi kuitawala Zanzibar.
Akitoa shukrani kwa Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale Zanzibar baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi Waitara alisema ziara hiyo ya kimafunzo imekuwa elimu kubwa kwa bodi na menejimenti kuona namna bora ya kuibua na kusimamia vivutio vya kihistoria, malikale na utalii katika visiwa na kuongeza vionjo kwa watalii hivyo kuongeza mapato yatokanayo na utalii nchini.
“Tumepata elimu kubwa ya maeneo haya adhimu ya kihistoria. Ziara hii imeboresha uhusiano ikizingatiwa kuwa Hifadhi za Taifa zinasimamia maeneo yenye mfanano kama maeneo ya Zanzibar, tutaendelea kushirikiana katika kuhifadhi maeneo haya ya Visiwa kwa faida ya vizazi vijavyo.”
Naye Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara, Massana Mwishawa kwa niaba ya Menejimenti alisema “Hivi karibuni tumefungua ofisi kiunganishi hapa Zanzibar ambayo itasaidia wageni kupata taarifa na kuweza kutembelea kwa wingi katika Hifadhi za Taifa hususan maeneo ya malikale pamoja na Hifadhi zilizopo karibu ambazo ni Hifadhi ya Taifa Saadani, Nyerere na Mikumi”
Ziara ya Bodi ya Wadhamini ya TANAPA visiwani Zanzibar imeangazia umuhimu wa kuunganisha historia, utamaduni, na uhifadhi wa katika kukuza utalii. Kutembelea Kisiwa cha Prison na Makumbushoyaliyopo Stone Town kumetoa fursa ya kujifunza jinsi vivutio hivi vinavyoendeshwa, sambamba na kuimarisha ushirikiano kati ya TANAPA na wadau wa utalii Zanzibar. Hii ni hatua muhimu katika kufanikisha juhudi za TANAPA za kuvutia watalii zaidi kwenye Hifadhi za Taifa, hasa zile zinazofanana na vivutio vya visiwani.