Featured Kitaifa

WAZIRI SIMBACHAWENE AWAASA WAHITIMU KUTUMIA TAALUMA ZAO VYEMA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewaasa wahitimu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kutumia vyema taaluma na ujuzi waliopata kwa manufaa yao na taifa kwa jumla.

Mhe. Simbachawene amesema hayo leo katika sherehe za Mahafali ya 40 ya kuwatunuku wahitimu wa ngazi mbalimbali katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika katika ukumbi wa Mkapa jijini Mbeya.

“Kuhitimu ngazi za Shahada, Stashahada, Astashahada na Astashahada ya Awali katika fani mbalimbali sio jambo dogo, elimu mliyopata ni kubwa, tumieni elimu hiyo kwa manufaa yenu na ustawi wa taifa” alisema Mhe. Simbachawene.

Aliongeza kuwa, ukuaji wa taifa lolote unategemea uwepo wa rasilimaliwatu imara na yenye weledi wa kutosha. Hivyo, amewataka wahitimu hao, kuepuka rushwa, ufisadi na kujikinga na ugonjwa hatari wa UKIMWI na magonjwa mengine yasiyoambuza kwa kuwa Taifa linawahitaji kwa ustawi imara.

Ameongeza kuwa, kuhitimu katika fani yoyote ile ni matokeo ya jitihada za muda mrefu si kwa wahitimu wenyewe tu bali pia hata kwa wale waliowasaidia kufikia hatua hiyo ikiwa ni pamoja na walimu, wazazi na walezi.

Vilevile, ameueleza Uongozi wa chuo kutambua kuwa Serikali ina matarajio makubwa na Chuo hicho hasa katika kuwajengea uwezo watumishi wa Umma na kutoa wahitimu wenye umahiri, uzalendo na tabia njema na hivyo kujenga uchumi wa nchi endelevu.

Awali, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Dkt. Ernest Mabonesho alimshukuru Mhe. Simbachawene kwa kukubali mwaliko wao na kumtarifu kuwa pamoja na jitihada nyingine zinazofanywa na chuo pia, chuo kimeendelea na juhudi za kufufua na kuanzisha ushirikiano na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuboresha ujuzi na kubadilishana uzoefu.

“Ili kuboresha mafunzo yetu, tumeona hainabudi kushirikiana na vyuo vingine vya nje na ndani ya nchi hususani vinavyohusika na masuala ya Utumishi wa Umma ili kuweza kupata fursa ya kujifunza na kutoa mafunzo bora zaidi” alisema Dkt. Mabonesho.

About the author

mzalendoeditor