Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS KUZINDUA MPANGO WA MAKAZI KWA WATUMISHI WA UMMA

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa Mpango wa Makazi kwa watumishi wa umma Disemba 11, 2024 katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma.

Na.Alex  Sonna-DODOMA

MAKAMU wa Rais Dk. Philp Mpango, anatarajiwa kuzindua Mpango wa Makazi kwa watumishi wa umma Disemba 11, 2024 katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma wenye lengo kutatua changamoto za makazi kwa watumishi.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, alibainisha hayo jana jijini hapa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa Mpango huo.

“Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma ulianza kutekelezwa mwaka 2014 chini ya usimamizi wa Watumishi Housing Investments (WHI) na hadi sasa, zaidi ya nyumba 1,000 zimejengwa katika mikoa 19 nchini Tanzania, ikiwemo Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Morogoro, Simiyu  Mtwara,”alisema

Aidha, alisema Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuboresha ustawi wa watumishi wa umma, kuhakikisha wanapata makazi bora, yenye gharama nafuu na salama.

“Kupitia mpango huu, watumishi wa umma wanapata fursa ya kumiliki nyumba kwa masharti nafuu, hatua inayolenga kuboresha hali ya maisha na kuongeza ufanisi kazini.

“Aidha mpango huu unalengo la kuwawezesha wananchi na hasa watumishi wa umma kiuchumi kupitia umiliki wa nyumba,”alisema Senyamule

Vilevile, alisema Watumishi Housing Investments kupitia mpango huo imetoa mikopo yenye masharti nafuu kwa watumishi wa umma ili kuwawezesha kumiliki nyumba kwa urahisi zaidi.

“Utekelezaji wa Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma ni dhamira pana ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata fursa ya kumiliki makazi bora,”alisisitiza

Kadhalika, alisema Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, inawaalika Watanzania wote kushiriki katika hafla hiyo muhimu ambayo inaashiria hatua kubwa katika kuboresha maisha ya watumishi wa umma na maendeleo ya sekta ya makazi nchini.

“Hafla hii si tu uzinduzi wa Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma, bali pia ni fursa ya kuonyesha mshikamano wa kitaifa katika kutatua changamoto za makazi na kuimarisha ustawi wa jamii,”alisema

About the author

mzalendoeditor