Featured Kitaifa

MRAJISI AIPONGEZA TTCL KWA KUANZISHA HUDUMA YA MALIPO KWA MKUPUO

Written by mzalendoeditor

Na Okuly Julius Dodoma

Mrajisi wa vyama vya ushirika nchini Dkt Benson Ndiege ameipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa kuanzisha huduma ya malipo kwa mkupuo kwa vyama vya ushirika.

Akizungumza mara baada ya kutembelea maonesho ya Wakulima Nanenane katika viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma amesema huduma hiyo imekuja wakati muafaka na itakuwa mkombozi kwa wakulima nchini.

“Kwenye vyama vya ushirika tuna vyama vya ushirika vya kilimo,kifedha madini vya mifugo na maeneo mengine yote kwa hiyo huduma hiyo itakuwa na tija kubwa”,Amesema.

Amesema kwenye vyama vya ushirika kuna watu zaidi ya 500 ambao wanalima zao linalofanana hivyo wanapohitaji kulipana njia ya malipo ya mkupuo itawasaidia zaidi.

“Mfumo huu unaenda kuwasaidia vyama vyote vya ushirika kwani ni njia salama na ya kuaminika na itasaidia katika utendaji kazi”,Amesema.

Aidha Dkt Ndiege ameongeza kuwa kutokana na umuhimu wa huduma hiyo wanapanga kukutana na uongozi wa TTCL na kuangalia jinsi huduma hiyo itakavyoenda kuwanufaisha vyama vya ushirika nchini.


About the author

mzalendoeditor