Featured Kitaifa

TUNA UMEME WA KUTOSHA SASA NA MIAKA KADHAA MBELE-MHANDISI MRAMBA

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema kuwa vyanzo vya umeme vilivyopo nchini vinazalisha umeme unaotosheleza mahitaji ya sasa na ya miaka kadhaa mbele.

Mha. Mramba amesema hayo wakati alipotembelea Maonesho ya Kimataifa ya Biashara (DITF) yanayoendelea jijini Dar es Salaam na kujionea shughuli zinazofanywa na Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zake.

“ Vyanzo vyetu vya umeme kama vile mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) vinazalisha umeme unaotosheleza mahitaji ya sasa na miaka kadhaa ijayo lakini sisi Wizara ya Nishati hatujipi likizo, wakati umeme huu ukiwa unatosha ndio wakati sahihi wa kuwekeza kwenye vyanzo vingine, hatutaki kurudi kwenye historia ya kutokuwa na umeme wa kutosha.” Amesema Mha.Mramba

Kutokana na uwepo wa umeme wa kutosha, Mha.Mramba amewaasa Watanzania kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kubuni miradi mbalimbali ya kujiletea maendeleo.

Aidha, ameeleza kuwa, kwa sasa nguvu kubwa imewekwa kwenye uzalishaji umeme unaotokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo nishati jadidifu ambapo ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni mradi wa umeme jua wa Kishapu (150MW) na miradi ya umeme wa upepo Singida na Makambako ambayo kwa pamoja itazalisha umeme wa kiasi cha megawati 300 hadi 400.

Ametaja vyanzo vingine vya umeme kuwa ni pamoja na vya Mto Malagarasi (49.5 MW), Kakono (87MW), Mto Songwe (180.2MW), Rumakali (222MW), Ruhudji (358MW) na bila kusahau chanzo cha Gesi Asilia ambacho kina uhakika wa kuzalisha umeme wakati wa mvua na usio wa mvua.

Katika hatua nyingine, Mha. Mramba amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kujiimarisha kiutendaji na hivyo kupelekea nchi kuwa na umeme unaotosheleza mahitaji na zaidi.

“TANESCO katika siku za hivi karibuni wamejitahidi sana kutekeleza majukumu yao, miezi michache iliyopita walibeba mzigo mkubwa wa Taifa kuhakikisha kuwa nchi ina umeme wa kutosha, baada ya juhudi kubwa sasa umeme upo wa kutosha na kuzidi matumizi.” Ameeleza Katibu Mkuu

Hata hivyo, amelitaka Shirika hilo kuongeza ubunifu ili kuweza kutoa huduma ya umeme kwa ubora zaidi na gharama ndogo zaidi.

“Nimezungumza nao kuhusu utafiti katika sekta ya umeme duniani kuangalia wenzetu wanatumia teknolojia gani mpya, vifaa gani vipya ambavyo vinaboresha huduma ya umeme na kupunguza gharama, mfano eneo la kutafuta mifumo ya umeme ambayo itapunguza ukataji wa miti, kwani miti iliyopo chini ya nyaya za umeme zenye umeme mdogo hulazimika kukatwa na hii inaathiri mazingira.” Amesema Mha.Mramba

Kuhusu utekelezaji Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ametaka Taasisi za Serikali pamoja na wadau kuendelea na ubunifu ambao utapunguza gharama za vifaa vya nishati hiyo ikiwemo majiko ya umeme kwani ndizo bidhaa zinazogusa maisha ya watu moja kwa moja na kuagiza kuwa elimu ya Nishati Safi ya Kupikia izidi kutolewa kwa makundi mbalimbali ya wananchi.

About the author

mzalendo