Featured Kitaifa

USAWA WA KIJINSIA NI CHACHU YA MAENDELEO YA TAIFA – DKT. MZURI

Written by mzalendo


Na WMJWMM-Dar es salaam.

Mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kizazi chenye Usawa (GEF) Dkt. Mzuri Issa amesema uwezashaji kwa wanawake kielimu na kiuchumi ndiyo madaraja pekee ya kufikia usawa wa Kijinsia nchini.

Ameyasema hayo katika ziara ya Kamati hiyo yenye lengo la kutambua utekelezaji wa Programu na jitihada zilizopo za kukuza haki na usawa wa kiuchumi kwa wanawake nchini Julai 09, 2024, Jijini Dar Es Salaam.

Dkt. Mzuri amesema mwamko kwa mabinti kielimu hususani katika michepuo ya sayansi ni kiashiria kizuri kuwa Jamii inaelekea kutimiza ahadi zilizowekwa na Mhe.Rais Dkt Samia Hassan kufikia kizazi chenye Usawa .

“Awali masomo ya sayansi yalichukuliwa kuwa ni masomo kwa ajili ya wanaume peke yake lakini sasa mtazamo ni tofauti kwani mabinti wengi hawaogopi tena kusoma masomo ya sayansi yote hayo yakiwa ni matokeo ya juhudi za serikali katika kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake ikiwemo kujenga shule maalum zinazofundisha Masomo hayo.” amesema Dkt Mzuri.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Uwekezaji wa Mamlaka inayosimamia uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) James Maziku amesema viwanda vinavyozalisha mavazi vimeweza kutoa ajira kwa Makundi yote ya Wanaume na Wanawake hivyo kuwapa fursa pia Wanawake kujikwamua kiuchumi.

“Kiwanda cha Tooku Garment kimeweza kutoa ajira zaidi ya 4000 na asilimia zaidi ya 80 ni wenye jinsia ya kike na hii inasaidia wanawake kupunguza wimbi la umaskini na utegemezi lakini pia kupata ujuzi wa ushonaji wa mavazi ya suruali (jeans) ambayo ni mavazi yanayovaliwa ulimwenguni kote” amesema Ezekiel.

Kwa upande wake mmoja wa wanufaika wa mikopo ya Serikali inayotolewa kupitia benki ya CRDB na mwenyekiti wa kikundi cha Bunju Women, Jackline Mkina ameipongeza Serikali kwa kuwainua kiuchumi kupitia mitaji wezeshi yenye riba nafuu pamoja na elimu kwa wanawake juu ya ujasiriamali.

“Kwa kuwa Mheshimiwa Rais hawezi mfikia kila mwanamke hivyo sisi viongozi wa vikundi ni wasaidizi wake na tunapaswa kuwaongoza wanakikundi ipasavyo ili kuwasaidia kufikia malengo ya kukua kiuchumi na kujikomboa na umaskini” amesema Jackline.

About the author

mzalendo