Featured Kitaifa

MATUMIZI YA STAKABADHI ZA GHALA YANACHOCHEA USHINDANI WA BEI ZA MAZAO SOKONI

Written by mzalendo

Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unachangia kuongeza thamani ya mazao na kuwezesha kupata bei zenye ushindani zinazoleta tija na faida kwa Wakulima na Jamii.

Kauli hiyo imetolewa leo Julai 4, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Mhe. Zakaria Mwansasu, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwenye Siku maalum ya Stakabadhi za Ghala wakati wa Maadhimisho ya Ushirika Duniani yanayofanyika katika Viwanja vya Ipuli, Mjini Tabora.

Mhe. Mwansasu amesema hadi kufikia Machi 2024, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala imeratibu ukusanyaji wa mazao kilogramu milioni 371 yenye thamani ya shilingi Bilioni 905.

Baadhi ya mazao yaliyohusika katika Mfumo huo ni pamoja na Mbaazi kwa Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma na Manyara ambayo yaliingiza Shilingi Bilioni 1.6 kwa Halmashauri za Mikoa hiyo na mapato kwa mkulima shilingi Bilioni 94.6; Kakao kwa Mikoa ya Morogoro na Mbeya ambazo yalizipatia Shilingi Bilioni 1.4 Halmashauri za Mikoa hiyo na mapato kwa mkulima Shilingi Bilioni 102.9 kwa mkulima; Korosho kwa Mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Ruvuma na Morogoro ambayo ilizipatia Shillingi Bilioni 7 kwa Halmashauri za Mikoa hiyo na mapato kwa mkulima shilingi Bilioni 407.9.

Akiongea katika Kongamano la Stakabadhi ya Ghala, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi ya Ghala, Asangye Bangu, amesema Bodi hiyo inaendelea kuimarisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa kutoa rai ya kuongeza matumizi ya mizani za kidijitali pamoja na matumizi ya TEHAMA.

Kwa upande wake Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, ametoa wito kwa Wanaushirika kukusanya mazao yenye ubora ili kuepusha usumbufu kwa wanunuzi na Mfumo mzima wa Stakabadhi ya Ghala.

   

About the author

mzalendo