Featured Kitaifa

UHALIFU SIO DILI KILA MMOJA AUCHUKIE UHALIFU

Written by mzalendo

Wananchi wa Kata ya Itumpi Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wametakiwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika suala la ulinzi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili jamii iwe salama.

Hayo yalisemwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga Juni 07, 2024 alipotembelea Kata hiyo kwa lengo la kutoa elimu ya umuhimu wa ulinzi jirani na madhara ya uhalifu na wahalifu katika jamii.

Kamanda Senga alisema kuwa “kila mwananchi akichukia vitendo vya kihalifu na kushirikiana na Jeshi la Polisi katika suala la ulinzi wa mali zetu ni dhahiri jamii yetu itakuwa salama kwa ustawi wa kila familia na jamii kwa ujumla” alisema Kamanda Senga.

Kamanda Senga aliwataka wananchi hao kushirikiana na viongozi wa maeneo yao kukemea vitendo viovu vinavyotokea katika jamii ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za wageni wanaofika katika kata hiyo ili kuweza kutambulika, kwani baadhi wamekuwa wakiwapokea watu na baadae kufanya vitendo vya kihalifu nakutokomea bila kuwa na taarifa zake.

About the author

mzalendo