Na. James Mwanamyoto, OR-TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde amesema, mwalimu ni mzazi wa pili na mlezi wa watoto shuleni ambaye anatoa mchango mkubwa kwa taifa katika kuwaandaa watoto kuwa viongozi wa baadae na wataalam wabobezi ambao taifa linawategea katika kuleta maendeleo.
Dkt. Msonde amesema hayo, kwa nyakati tofauti wakati vikao kazi vyake na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo katika Halmashauri za Wilaya ya Kyerwa na Ngara zilizopo mkoani Kagera.
“Mwalimu ni mzazi wa pili na ndiye anayekaa na mtoto kwa muda mrefu zaidi kuliko wazazi wake wa kumzaa, anamlea na kumpatia maarifa na ujuzi utakao msaidia kuendesha maisha yake na kutoa mchango katika taifa,” Dkt. Msonde amesisitiza.
Dkt. Msonde amefafanua kuwa, mchango wa mwalimu ni namba moja nchini na ndio maana Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema licha ulezi wake mwalimu, lakini ndiye anawayewapatia ujuzi watoto ambao unaowajengea umahiri wa kuwa wataalam katika fani mbalimbali.
“Kila ambaye utakutana nae mtaani awe ni bwana shamba, bwana mifugo, mwanasheria, mhandisi au kiongozi yeyote utambue kuwa amefikia hapo alipo kwa sababu mwalimu amempatia ujuzi uliomwezesha kuwa mtu mwenye hadhi yake katika jamii,” Dkt. Msonde amesema.
Dkt. Msonde ameongeza kuwa, mwalimu ni mtu muhimu na wa thamani kubwa katika jamii na ndio maana akimuona mtu akimdhihaki au kumnyanyasa mwalimu anaumia na kutamani mamlaka husika zimchukulie hatua.
Dkt. Msonde amehitimisha ziara yake mkoani Kagera kwa kufanya vikao kazi na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo katika Halmashauri za Wilaya ya Kyerwa na Ngara, ambapo alitumia muda mwingi katika halmashauri zote alizozitembelea kuhimiza uwajibikaji kwa walimu ili mchango watakaoutoa uwe na tija katika maendeleo ya taifa.