Featured Kitaifa

SERIKALI KUTUMIA VIKAO RASMI KUTOA ELIMU YA FEDHA

Written by mzalendo

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Bw. Isaya Mbenje, akizungumza na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha (haipo pichani) ambayo ilifika ofisini kwake kujitambulisha na kuelezea njia watakazo tumia kufikisha elimu ya huduma ndogo za fedha katika Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.

Baadhi ya Wananchi wa Kisiwa cha Bumbire wakiangalia filamu yenye mada mbalimbali kuhusu elimu ya huduma ndogo za fedha ambayo ilitumika na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha kutoa elimu kwa wananchi wa makundi mbalimbali mkoani Kagera.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Bw. Isaya Mbenje, akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha, ambayo ipo mkoani Kagera kutoa elimu ya huduma ndogo za fedha. Kutoka kushoto ni Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bi. Mary Mihigo, Afisa Biashara na Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha Wilaya ya Muleba, Bw. Joseph Masawe, Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha Bw. Stanley Kibakaya na Afisa Mwandamizi Uchambuzi Masuala ya Fedha kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bi. Gladness Mollel.

Afisa Mwandamizi wa Uchambuzi wa Masuala ya Fedha kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Bi. Gladness Mollel, akitoa elimu kwa Wananchi wa Kisiwa cha Bumbire kuhusu masuala ya uwekezaji wilayani Muleba mkoani Kagera.

Timu ya Wataalam ya Wizara ya Fedha ikiwa tayari kuanza safari kuelekea Kisiwa cha Bumbire, wilayani Muleba mkoani Kagera, kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi wa Kisiwa hicho ambapo mada mbalimbali zilifundishwa ikiwemo utunzaji wa akiba na mikopo.

Picha ya Kisiwa cha Bumbire ambapo Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ilifika kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi wa Kisiwa hicho ambapo mada mbalimbali zilifundishwa ikiwemo utunzaji wa akiba na mikopo.

Mkazi wa Kisiwa cha Bumbire, Bw. Maka Osward, akiuliza swali kuhusu njia bora ya kuwekeza kwa Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ilifika Kisiwani humo kutoa elimu ya fedha ambapo iliwafundisha wananchi hao mada mbalimbali ikiwemo kujiwekea akiba, namna bora ya kukopa na uwekezaji.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Kagera)

NA: JOSEPHINE MAJULA, KAGERA

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Bw. Isaya Mbenje, amesema kuwa Serikali itaanza kutumia vikao vyake rasmi kutoa elimu ya huduma ndogo za fedha ili kupunguza migogoro inayoendelea nchini kuhusu mikopo na watu kuchukuliwa mali zao kwa kushindwa kulipa mikopo.

Bw. Mbenje alitoa ahadi hiyo wakati alipokutana na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ilifika Kisiwa cha Bumbire kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi wa Kisiwa hicho ili waweze kujikomboa kiuchumi.

“Nitahakikisha Waratibu wa Elimu Ndogo ya Fedha ngazi ya Wilaya wanapata muda wa kutoa elimu katika vikao rasmi vya Serikali ambavyo vinawahusisha watu wengi wakiwemo Waheshimwa Madiwani na watu wote ili waweze kufikisha elimu hii kwa watu wanaowasimamia”, alisema Bw. Mbenje.

Alisema kupitia Waheshimiwa Madiwani ambao ni Wawakilishi wa Wananchi katika ngazi ya Kata na Vijiji wakipewa elimu ya fedha vizuri na kuelewa itawafikia wananchi wengi katika maeneo yote kwa kuwa kila Kata na Vijijini inawawakilishi katika mikutano rasmi ya Serikali.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata wa Kisiwa cha Bumbire, Bw. Davis Alistedius, alisema kuwa kupitia elimu waliyoipata wananchi wa Kisiwa chake watahakikisha wanawasimamia waweze kusajili biashara zao ili ziweze kutambulika rasmi na Serikali ili kuwawezesha kufanya kazi kwa uhuru.

Naye mkazi wa Kisiwa cha Bumbire, Bw. Anorld Rweyemamu, aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kuwafikia na kuwapa elimu hiyo muhimu itakayowakomboa kiuchumi kupitia mada mbalimbali walizofundishwa ikiwemo uwekezaji, mikopo na umuhimu wa kuweka akiba.

“Elimu tuliyoipata ni nzuri ila tunaiomba Serikali iendelee kuwashawishi wawekezaji hususan Taasisi za Fedha kama benki kuja kuwekeza katika Kisiwa chetu ili kupitia Taasisi hizo tuweze kujiwekea akiba na kufanya uwekezaji kupitia ununuzi wa hisa”, alisema Bw. Rweyemamu.

Naye Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bi. Mary Mihigo, aliwashukuru Wananchi wa Kisiwa cha Bumbire kwa kujitokeza kwa wingi kupata elimu ya fedha ambayo itawasaidia kuwa na matumizi sahihi ya fedha kutokana na mada mbalimbali walizowafundisha ikiwemo usimamizi wa fedha binafsi.

Wizara ya Fedha inaendelea na zoezi la kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika mikoa nane ikiwemo Kagera, Singida na Manyara ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2021/2022.

About the author

mzalendo