Featured Kitaifa

TAFITI ZIJIBU CHANGAMOTO ZA SEKTA YA USHIRIKA 

Written by mzalendoeditor

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, amewataka Wataalamu pamoja na Wanaushirika kutumia Tafiti za Ushirika kutatua changamoto za Sekta ya Ushirika.

Ametoa agizo hilo wakati akifungua Kongamano la tatu la Tafiti na Maendeleo ya Ushirika Leo Mei 28, 2024 Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Mweli amesema ni muhimu kwa watendaji kufuatilia mapendekezo yanayotolewa katika Tafiti, kuyafanyia kazi ili kutatua changamoto zinazojitokeza katika Sekta ya Ushirika.

“Ni lazima tuweke mifumo yenye uwazi wa ufuatiliaji wa mapendekezo yenye matokeo yanayotokana na Tafiti,” amesisitiza.

Aidha, ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuendelea kushirikiana na wadau katika Tafiti, kuboresha usimamizi wa Vyama na kuimarisha matumizi ya teknolojia.

Kwa upande wake Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege amesema Tume itaendelea kuhakikisha Tafiti zinawafikia walengwa kwa Maendeleo ya Ushirika.

Katika kongamano hilo lililoshirikisha Wadau mbalimbali wa Ushirika, Benki ya Taifa ya Ushirika imekabidhiwa Cheti cha Usajili; na Mfuko wa Tafiti za Ushirika umezinduliwa rasmi.

About the author

mzalendoeditor