Featured Kitaifa

MFUMO WA “CHAMPION APP” KURAHISISHA UTOAJI WA ELIMU NGAZI YA JAMII

Written by mzalendo

Na Angela Msimbira, KATAVI

OFISI ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya imeanza majaribio ya mfumo utakaowezesha watoa huduma za afya ngazi ya jamii kutoa elimu ya masuala ya afya kwa umma.

Mfumo huo ujulikanao Champion APP umetengenezwa na wadau afya taasisi ya Girls Effect kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Wizara ya Afya na majaribio yanafanyika katika Halmashauri za Tanganyika, Mpimbwe na Nsimbo mkoani Katavi.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo kuhusu mfumo huo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Dkt. Alex Mrema amesema mfumo huo utawawezesha watoa huduma za afya ngazi ya jamii kutumia njia rahisi ya kufikisha ujumbe kwa haraka na kupata matokeo chanya katika kuimarisha huduma bora za afya kwa jamii.

“Watoa huduma za afya ngazi ya jamii ni muhimu na ni taswira ya afya, hivyo Serikali imetafuta mbinu ya kumuwezesha na kuandaa zana ili waweze kufanikiwa katika utoaji wa elimu kwa jamii katika ngazi ya jamii, hivyo kwa kutumia mfumo huo watatumia njia rahisi itakayowezesha kufikisha ujumbe kwa haraka na kupata matokeo chanya katika kuimarisha huduma bora za afya kwa jamii.”

Amesema kwa sasa watoa huduma za afya ngazi ya jamii wamekuwa wamekuwa wakifikisha ujumbe wa afya moja kwa moja kwa wananchi wa kawaida kwa kutumia njia ya mawasiliano za jadi kama vile mazungumzo ya mdomo au ishara za kimwili njia ambazo zina faida kidogo hasa katika maeneo yenye wananchi wengi wasiojua kusoma na kuandika hivyo kuhathiri ufikaji na matumizi ya taarifa muhimu kwa wananchi.

Amesema utafiti umeonesha kuwa njia hizo zilikuwa haziwafiikii wananchi walioko kwenye maeneo ya pembezoni na wale wasiojua kusoma na kuandika na kutumia mfumo huo itatumika njia ya simulizi zitakazowekwa kwenye mfumo hatua ambayo itarahisisha utoaji wa elimu kwa jamii.

“Kuleta zana za kisasa za kufundishia zenye sauti kunaweza kubadilisha hali ya sasa na kufanya mawasiliano na elimu kuhusu masuala ya afya kuwa ya kuvutia zaidi na kupatikana kwa urahisi na kuongeza faida za uwepo wa watoa huduma za afya ngazi ya jamii.”

Januari 31 mwaka huu, Serikali ilizindua Mpango Jumuishi wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwa lengo la kuimarisha mifumo ya afya ngazi ya jamii na kurahisisha utoaji elimu ya afya kwa umma.

About the author

mzalendo