Featured Kitaifa

DKT.MPANGO ASHIRIKI MAADHIMISHO YA MIAKA 102 TANGU KUZALIWA BABA WA TAIFA

Written by mzalendo

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Miaka 102 tangu kuzaliwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma. Tarehe 13 Aprili 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mzee Paul Kimiti wakati alipowasili katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma kushiriki Maadhimisho ya Kitaifa ya Miaka 102 tangu kuzaliwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tarehe 13 Aprili 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Miaka 102 tangu kuzaliwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma. Tarehe 13 Aprili 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikabidhiwa tuzo na Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mzee Paul Kimiti kwaajili ya kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuliongeza Taifa kwa mafanikio makubwa mwaka 2021-2024. Tuzo hiyo imetolewa katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Miaka 102 tangu kuzaliwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma. Tarehe 13 Aprili 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akionesha tuzo iliyotolewa kwaajili ya kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuliongeza Taifa kwa mafanikio makubwa mwaka 2021-2024. Tuzo hiyo imetolewa katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Miaka 102 tangu kuzaliwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma. Tarehe 13 Aprili 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikabidhiwa tuzo na Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mzee Paul Kimiti iliyotolewa na Taasisi hiyo kupongeza jitihada za Makamu wa Rais katika Uhifadhi wa Mazingira. Tuzo hiyo imetolewa katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Miaka 102 tangu kuzaliwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma. Tarehe 13 Aprili 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa Mataifa ya Zimbabwe, Namibia, Msumbiji na Uganda walioshiriki Maadhimisho ya Kitaifa ya Miaka 102 tangu kuzaliwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma. Tarehe 13 Aprili 2024.

……………

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania………..!

Kwanza, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutupatia nafasi kukutana leo kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 102 ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa letu la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye alizaliwa tarehe 13 Aprili 1922 katika Kijiji cha Butiama, Mkoa wa Mara. Aidha, napenda kuishukuru na kuipongeza kwa dhati, Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius  Nyerere, kwa maandalizi mazuri na kwa kunipa heshima kuwa mgeni rasmi katika kumbukizi hii. Nimefahamishwa kuwa, lengo kuu la maadhimisho haya ni kuwakumbusha na kuhamasisha vijana na watanzania wote umuhimu wa kushiriki katika kudumisha amani, kuhifadhi na kutunza mazingira, kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za Taifa na kutunza na kuenzi mchango wa Tanzania katika historia ya ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika ikiwemo katika Wilaya ya Kongwa na sehemu nyingine za nchi yetu. Aidha, maadhimisho haya yanalenga pia kumpongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuliongoza vema Taifa letu na kudumisha umoja, amani na mshikamano wa watanzania.

Napenda kuwapongeza tena waandaaji wa Kongamano hili kwa kuandaa Mjadala unaoshirikisha vijana wa shule za msingi, sekondari na vyuo ili kujadili umuhimu wa kutunza amani, rasilimali za Taifa na mazingira kwa maendeleo endelevu ya nchi yetu. Naamini hili ni jambo ambalo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere angependa, kwa sababu ya umuhimu wa vijana katika uhai na uendelevu wa Taifa. Ni faraja kwangu kuwaona vijana wakishiriki Mijadala ya mambo muhimu ya kitaifa katika Kumbukizi hii ya Miaka 102 ya Baba wa Taifa. Kwa ajili hiyo, katika hotuba yangu siku ya leo, nitajielekeza katika kueleza nafasi ya kijana katika kudumisha amani, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za Taifa, utunzaji wa mazingira na kutunza historia ya ukombozi kusini mwa Afrika.

Kwanza, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alianza harakati za ukombozi wa Taifa letu akiwa kijana. Kumbukumbu zinaonesha kuwa Mwalimu alianza harakati za kisiasa akiwa na umri wa miaka 20  tu au hata kabla ya hapo. Harakati zake za kisiasa ziliwezesha kuzaliwa Taifa huru la Tanganyika mnamo tarehe 09 Disemba 1961 akiwa kijana wa miaka 39 tu. Aidha, kutokana na uongozi wake alisaidia kufanikisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuzaliwa Taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kupitia kipawa kikubwa cha uongozi alichojaliwa na Mwenyezi Mungu, Baba wa Taifa aliweza kuunganisha makabila zaidi ya 120 yaliyokuwa chini ya tawala za kimila na kuwa Taifa moja. 

Aidha, katika Serikali yake, Mwalimu Nyerere aliwaamini viongozi vijana (wanaume na wanawake) na kuwateua kushika nafasi mbalimbali za uongozi. Baadhi ya vijana hao ni pamoja na: Mhe. Balozi Dkt. Salim Ahmed Salim, ambaye aliteuliwa kuwa Balozi nchini Misri akiwa na miaka 22 tu, Mzee wetu Mhe. Paul Kimiti aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro akiwa na miaka 44, Bibi Titi Mohamed ambaye alianza kushiriki harakati za kisiasa akiwa na miaka 24 tu na kufanya kazi na Mwalimu na Mhe. Pius Msekwa ambaye alianza kushika nafasi za uongozi akiwa na miaka 25 tu. Vilevile, Baba wa Taifa alianzisha JKT ili kujenga maadili kwa vijana na kuwawezesha kuleta amani, kulinda nchi yao na rasilimali za Taifa. Kwa vijana mlioko shuleni na kwenye vyuo nawasihi msome  kwa bidii ili kujiwekea msingi imara na malengo ya kufikia ndoto zenu kama Baba wa Taifa alivyokusudia. Maendeleo ya Taifa lolote duniani yanategemea vijana na ushiriki wao katika  shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo uongozi. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu 2024 na Uchaguzi Mkuu wa Rais na wabunge na madiwani 2025 ni fursa nzuri kwa vijana wenye sifa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Pili, Baba wa Taifa alisisitiza umuhimu wa elimu hasa kwa vijana katika kupambana na umasikini. Katika moja ya hotuba zake alisema maadui watatu wa Taifa letu ni ujinga, maradhi na umasikini. Wakati wa uongozi wake alianzisha programu ya kuhakikisha watanzania wote wanajua kusoma na kuandika. Aidha, katika kusisitiza umuhimu wa elimu, Mwalimu Nyerere alieleza kuwa elimu siyo njia ya kuepukana na umasikini bali ni njia ya kupambana nao. Mwalimu Nyerere aliwataka vijana wa kitanzania wanaopata fursa ya kusoma, kuhakikisha wanatumia elimu yao kwa manufaa ya watanzania. Katika moja ya Hotuba zake alifananisha kijana anayepata fursa ya kusoma na mtu anayetumwa nchi ya mbali kwenda kutafuta chakula kwa ajili ya kijiji/familia. Alieleza kuwa endapo mtu huyo atafika sehemu akapata chakula hicho na kusahau kurudi kwa waliomtuma atakuwa amefanya kosa kubwa. Kwa ajili hiyo, aliwataka vijana kuhakikisha wanasoma kwa bidii na kutumia elimu wanayoipata kwa manufaa ya watanzania wote. Naomba kutumia fursa hii kuwaeleza vijana wa kitanzania mliopo hapa siku ya leo kuwa mnayo nafasi kubwa ya kujiendeleza kielimu kwa manufaa ya Taifa letu. Wazazi na Taifa kwa ujumla tunawategemea msome kwa bidii na kutumia maarifa mtakayoyapata kutatua changamoto mbalimbali katika jamii yetu. Katika zama hizi zinazotawaliwa na maendeleo ya kasi ya sayansi na teknolojia, ninawahimiza vijana wa kitanzania msibakie nyuma kutafuta maarifa katika tasnia zinazoibuka ikiwemo akili mnemba (Artificial Intelligence), robotic engineering, matumizi ya teknolojia ya kidigitali na fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia ya habari.

Tatu, Mwaka huu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utatimiza miaka 60. Katika kusherehekea miaka 60 ya Muungano tunayo kaulimbiu inayosema: MIAKA 60 YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, TUMESHIKAMANA NA TUMEIMARIKA KWA MAENDELEO YA TAIFA LETU. Sasa kulingana na Takwimu zinazotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, asilimia 94 ya watanzania wamezaliwa baada ya Muungano. Aidha, kwa mujibu wa Sensa hiyo, asilimia 77.3 ya watanzania ni vijana wenye umri wa chini ya miaka 35. Swali la kujiuliza hapa ni vijana wangapi mnauelewa wa kutosha kuhusu Muungano wetu? Je vijana mnazitambua faida za Muungano na sababu zilizopelekea kuundwa kwa muungano? Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, aliasisi na kudumisha Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili. Muungano wetu umejengwa katika dhana kuu ya Umoja wa kitaifa. Wakati wa uhai wake Mwalimu alituasa kuulinda Muungano wetu na kutatua changamoto za muungano zinazojitokeza kwa njia ya mazungumzo. Katika moja ya hotuba zake, Baba wa Taifa alifananisha Muungano wetu na nyumba iliyojengwa na kisha kupata nyufa. Alituasa kuziba nyufa za Muungano badala ya kuubomoa Muungano wenyewe. Alikemea ubaguzi wa aina yoyote ambao ungeweza kupelekea kuvunjika kwa Muungano. Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kushughulikia changamoto za Muungano. Katika kipindi cha takribani miaka mitatu ambacho Mheshimiwa Rais amekuwa madarakani, jumla ya changamoto za Muungano 15 zimefanyiwa kazi na kupatiwa ufumbuzi. Aidha, changamoto zilizosalia zinaendelea kufanyiwa kazi. Napenda kutumia fursa hii, kuwapa changamoto vijana wote wa kitanzania kufanya jitihada za kuelewa misingi na faida za muungano na kuwa mstari wa mbele katika kuulinda na kuuenzi muungano wetu adhimu.

Nne, Maadhimisho ya mwaka huu yanalenga pia kutambua na kuenzi mchango wa Tanzania katika ukombozi wa  nchi za kusini mwa Afrika hususan Msumbiji, Zimbabwe, Afrika Kusini, Namibia na Angola ambazo wapiganaji wake walikuwa na makazi yao hapa nchini. Katika mwongozo alioutoa kuhusu Utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania (Argue don’t shout, An Official Guide on Foreign Policy by the President, July 1969) Mwalimu Nyerere alieleza malengo ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania kuwa ni kulinda uhuru wetu, kujenga nchi ya kijamaa, kusaidia kuzikomboa Nchi za Kusini mwa Afrika na kuhamasisha Umoja wa Afrika. Katika Mwongozo huo, Mwalimu aliwataka watanzania kujenga hoja katika kuelezea malengo ya Sera yetu ya Mambo ya Nje. Sehemu ya Mwongozo huo inasomeka kwa kiingereza kama ifuatavyo: 

“Tanzania has definite viewpoints on foreign affairs. We have to state firmly what they are, why we have adopted them, and what they mean. We must do this because, in conformity with our objectives, we want either to influence people, or to have them understand why we have adopted a particular line of action. And for either of these purposes, we have to argue our case, not just shout. It is relevant to remember that, when a speaker screams into a microphone, the audience hears only a bubble of unpleasant noise – it cannot hear what is being said and is unlikely to make any effort to do so.”

Ni kutokana na msimamo na mwongozo huo, Tanzania ilijitolea kuzisaidia nchi za Kusini mwa Afrika kupigania uhuru wake ikiwa ni pamoja na kutoa maeneo ya kujenga kambi za wapigania uhuru katika Ardhi ya Tanzania. Aidha, Tanzania ilitumia majukwaa mbalimbali ya kimataifa kujenga hoja kupinga ukoloni na ukandamizaji wa nchi za Kusini mwa Afrika mpaka nchi hizo zilipopata uhuru wake. Vilevile, Tanzania ilikuwa tayari kutoa fedha, zana za kivita, askari na mafunzo kwa ajili ya wapigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika. Baada ya ukombozi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaendelea kuimarisha uhusiano na nchi zote za Kusini mwa Afrika kupitia Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kupitia mahusiano ya pande mbili ya kidiplomasia na kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili. Aidha, Serikali inaendelea kufanya juhudi mbalimbali kutunza historia adhimu na mchango wa Tanzania katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika. Kwa mfano Serikali imeamua kukarabati kambi ya wapigania uhuru katika Wilaya ya Kongwa. Vilevile, kambi ya wapigania uhuru ya Mazimbu, Morogoro sasa yanatumika kama sehemu ya Kampasi za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo. Ni muhimu kwa vijana wa kitanzania kuelewa kuwa Tanzania ilishiriki ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika kwa kutambua kuwa uhuru na usalama wetu wenyewe unategemea pia uhuru wa nchi nyingine za Afrika.

  

Tano, Baba wa Taifa alihimiza matumizi ya kiswahili na kudumisha utamaduni wa mtanzania.  Mwalimu alitumia lugha ya Kiswahili kuwaunganisha watanzania wakati wa kupigania uhuru na baada ya kujitawala. Mwaka 1962, Serikali ikiongozwa na Mwalimu Nyerere iliridhia Kiswahili kitumike Bungeni na katika shughuli zote za Serikali. Mwaka 1964 alianzisha Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) na Kiswahili kilitangazwa kuwa lugha ya Taifa.  Mwaka 1965 lugha ya Kiswahili iliteuliwa kuwa lugha ya kufundishia masomo yote na lugha ya kiingereza ilibakia kuwa somo. Mwaka 1967 Serikali ilianzisha Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kwa lengo la kuchagiza maendeleo ya Kiswahili nchini. Aidha, kama hiyo haitoshi,  Baba wa Taifa alikuza na kuendeleza Kiswahili kupitia uandishi wa vitabu na kufasiri vitabu kwa lugha ya Kiswahili. Vitabu vilivyoandikwa na Baba wa Taifa ni pamoja na: Ujamaa kama Msingi wa Usoshalisti; Demokrasia na Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa; TANU na Raia; na Tujisahihishe. Aidha, Baba wa Taifa alifasiri Tamthilia ya The Merchant of Venice ya William Shakespeare kwa Kiswahili kuwa “Mabepari wa Venisi.” Vilevile, Mwalimu aliandika utenzi wa Injili za Yohana, Marko na Mathayo na Kitabu cha Matendo ya Mitume kwa kiswahili. Ni kutokana na jitihada hizo za awali za Baba wa Taifa kukuza lugha ya Kiswahili, zimepelekea lugha hii imeendelea kupata heshima duniani kote. Hivi sasa, Kiswahili ni lugha rasmi ya Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Aidha, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeitenga siku ya tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani.  Hivyo, vijana wa kitanzania mnayo nafasi ya pekee kujivunia lugha ya kiswahili na utamaduni wa mtanzania. Zipo fursa nyingi sasa zinazotokana na matumizi ya lugha ya Kiswahili duniani. Fursa hizo ni pamoja ukalimani, uandishi wa vitabu vya kiada na ziada na vitabu vingine, ufundishaji wa kiswahili katika nchi mbalimbali, tafsiri ya vitabu vya lugha nyingine kwa kiswahili na matumizi ya kiswahili katika sanaa na muziki. Natoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa hizo kwa manufaa ya kijamii na kiuchumi. Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuchukua hatua madhubuti zenye lengo la kuendelea kukuza na kubidhaisha lugha ya Kiswahili kwa manufaa ya watanzania wote.

Sita, Baba wa Taifa alijipambanua kwa mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwa nchi yake na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alikuwa mzalendo wa kweli. Akiwa Mwalimu wa Shule ya St. Francis College Pugu, Mwalimu Nyerere alitakiwa kuchagua kati ya kazi yake ya ualimu na shughuli zake za kisiasa kupitia TANU. Kutokana na uzalendo wake kwa Taifa, Mwalimu Nyerere aliamua kujiuzulu kazi yake ya ualimu  ili apate muda zaidi wa kupigania uhuru wa Taifa letu. Katika barua ya kujiuzulu aliyomwandikia Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Baba wa Taifa  alisema “Nimetafakari chaguo ulilonipa kati ya kazi yangu shuleni na uanachama wangu katika TANU na nimefikia uamuzi kuwa lazima nijiuzulu katika nafasi yangu shuleni.” Aidha, katika uongozi wake Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alijipambanua kama kiongozi mwenye uzalendo mkubwa kwa nchi yake kwa kutunga sheria kali dhidi ya vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi, kuongoza Taifa katika vita vya Kagera dhidi ya majeshi ya Iddi Amin wa Uganda yaliyovamia nchi yetu, kusimamia matumizi endelevu ya rasimali za Taifa na kulinda amani na uhuru wa nchi yetu. 

Saba, Baba wa Taifa alilinda na kuhifadhi rasilimali za Taifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.  Katika moja ya hotuba zake Hayati Mwalimu Nyerere alisisitiza umuhimu wa kulinda maeneo ya hifadhi kwa kusema yafuatayo: “Tunayo maeneo ya hifadhi ambayo yanahifadhiwa kisheria, ambayo sasa tumeanza kulegeza ulinzi wake. Sasa nadhani kazi ya kwanza kabisa ambayo Serikali inapaswa ifanye, na humu wamo viongozi wetu wa Serikali za Mitaa, ni kukaza amri. Sheria zile zipo, kwamba maeneo yale ambayo yanahifadhiwa kwa mujibu wa sheria yaendelee kuhifadhiwa kwa mujibu wa sheria. Na yeyote atakayevunja sheria tupambane naye kwa sababu anatufanyia jambo la dhambi kabisa, jambo baya sana.” Vilevile, katika moja ya hotuba zake, Mwalimu Nyerere aliwahi kumfananisha mtu anayeharibu mazingira na mtu anayeiba mali za vizazi vingine. Alieleza kuwa kuharibu mazingira ni kudhulumu haki ya watoto na wajukuu wa vizazi vijavyo. Kwa ajili hiyo, ulinzi wa rasilimali za Taifa na mazingira yetu ni jukumu la vijana. Kila kijana wa kitanzania anao wajibu wa kulinda maliasili za Taifa kwa maendeleo endelevu ya Tanzania. Nazikumbusha pia Mamlaka za Hifadhi za Taifa na watanzania wote kuongeza jitihada za kulinda hifadhi zetu na kutunza mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Nane, Baba wa Taifa alitambua na kuhimiza kulinda amani katika Taifa. Kupitia hotuba zake, Mwalimu Nyerere alitusisitiza watanzania kuishi kwa amani na kuepuka ubaguzi kwa misingi ya rangi, dini, itikadi za kisiasa au kabila. Mwalimu alituasa kuwa na umoja na mshikamano ili kuweza kufanya kazi na kujiletea maendeleo. Kwa ajili hiyo, Mwalimu Nyerere aliwezesha  watanzania kuishi mahali popote nchini na kushirikiana. Aidha, Mwalimu Nyerere alitumia kipawa chake cha uongozi kusuluhisha migogoro ya mataifa mengine hususan Burundi, Rwanda na Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuhakikisha amani inarejea katika mataifa hayo. Aidha, wakati wa uongozi wake, Tanzania ilikuwa tayari kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi waliokimbia mapigano katika nchi zao. Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kudumisha amani kwa kuendeleza misingi iliyowekwa na Baba wa Taifa. Naomba kutumia fursa hii, kuwasihi watanzania hususan vijana kutokukubali kugawanywa kwa misingi ya itikadi za kisiasa, dini,  kabila au rangi na badala yake tuendelea kuwa na umoja na mshikamano kwa masilahi ya Taifa letu na vizazi vijavyo. 

Ndugu wageni waliakwa, mabibi na mabwana, kabla ya kumaliza Hotuba yangu, napenda kuungana na waandaaji wa Kumbukizi ya leo kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo kuliongoza Taifa letu katika misingi ya haki, usawa, amani, umoja na upendo. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kuendelea kulinda, kutunza na kuhifadhi Malikale ikiwa ni pamoja na zilizokuwa nyumba na kambi za wapigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika hapa nchini. Aidha, Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iangalie uwezekano wa kufanya kazi na wadau wengine kuangalia namna bora ya kuhifadhi kumbukumbu za Baba wa Taifa kama inavyofanyika kwa waasisi wa mataifa mengine.

Kama nilivyoeleza hapo awali siyo rahisi kueleza mazuri yote yaliyofanywa na  Mwalimu Nyerere katika hotuba moja. Ninaomba radhi kwa hotuba hii ndefu kidogo lakini naamini kwamba imekuwa ya manufaa kwa wasikilizaji wote. Nimalizie tu kwa kusisitiza kwamba sisi watanzania tunalo deni kubwa na wajibu wa kuendelea kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kuyaishi kwa vitendo yale mema yote aliyotufundisha kupitia uongozi wake na maisha yake. Tuendelee kuzilinda rasilimali zetu na mazingira kwa manufaa ya nchi yetu. 

Baada ya kusema haya, napenda kutamka kuwa Maadhimisho ya Kitaifa ya Kumbukizi ya Miaka 102 ya Kuzaliwa kwa Baba wa Taifa yamefunguliwa rasmi!

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Asanteni kwa kunisikiliza.

About the author

mzalendo