Featured Kitaifa

ACHENI TABIA YA KUSHIRIKIANA NA VIONGOZI WENU KUVUNJA SHERIA – PROF. MKUMBO

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo leo Machi 22,2024 amezindua Mkutano wa Baraza la Kwanza la Wafanyakazi wa hiyo lililoongozwa na kauli mbiu isemayo “Majadiliano yenye tija ni msingi wa ufanisi katika kazi.

Akizungumza katika uzinduzi huo Prof. Mkumbo amewataka wafanyakazi hao kuacha tabia ya kushirikiana na viongozi kuvunja sheria bali wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya kazi iliyopo.

Aidha amesema kuwa ni fursa nzuri kwa wafanyakazi kujengewa utamaduni mzuri wa kitaasisi ikiwemo kuacha tabia ya kuwaogopa viongozi kwani kila mtu anayo fursa ya kutoa maoni pamoja na kushirikishwa kwenye maandalizi ya bajeti zinazopangwa na Wizara.

“Utamaduni mzuri ni kuwa wewe ni mkuu wa kitengo, mkuu wa Idara umepokea taarifa kuwa bajeti yetu imepitishwa nawewe unakuja kuwashirikisha watumishi wengine hii itasaidia kuongeza thamani na motisha kwa wafanyakazi wetu katika kutimiza majukumu yao,”amesema Prof. Mkumbo.

Sambamba na hayo amewasisitiza kuwa na upendo pamoja na ushirikiano, na kuwakumbusha kuwa hakuna sehemu walipoandika hivo vitu lakini ni muhimu wapendane kwani wao ni familia moja pia wasioneane vijicho.

“Moja ya sifa ya kiongozi ni kugawa neema kubwa na ndogo ndogo ili kuongeza motisha za utekelezaji wa majukumu yao, kwenye maisha ya utumishi usitafite cheo wacha cheo kikutafute, la muhimu kazi uliyonayo kwa kipindi hicho itendee haki na mifumo ya kiutendaji ipo na hii ndiyo tabia ya kuoneana vijicho,”ameongeza.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida amesema Baraza lililozinduliwa leo litasaidia kusimamia vyema maslahi ya wafanyakazi na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaridhisha.

“Nikuhakikishie Mhe. Waziri kuwa kila mtumishi atahimizwa kutoa mawazo kwa lengo la kuongeza tija, ufanisi na kutoa huduma bora kwa gharama nafuu,”amesema.

Pia ameongeza kuwa Baraza hilo lililozinduliwa leo litasaidia kusimamia vyema maslahi na stahili za watumishi na kuishauri Ofisi kuhusu namna ya kubuni Sera na mipango ya kuwavutia wawekezaji.

Akitoa neno la shukrani Naibu Katibu Mkuu TULGHE Taifa Mhandisi Amani Msuya amempongeza Prof. Mkumbo kwa kuzindua baraza hilo na kuongeza kuwa moja kati ya kitu ambacho Waziri huyo anahitaji ni kuona matokeo chanya katika utendaji kazi.

About the author

mzalendo