Featured Kitaifa

ANDAENI MPANGO WA UFADHILI WATAALAMU WA KISWAHILI-MAJALIWA

Written by mzalendo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia, iandae mpango maalum wa ufadhili wa wataalam wa lugha ya Kiswahili kwenye ngazi ya shahada ya uzamivu ili kukidhi mahitaji sambamba na kuimarisha mafunzo ya lugha kwa ajili ya kuzalisha wataalam na wakalimani wa kiswahili wenye viwango vya kimataifa.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumatatu, Machi 18, 2024) wakati alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Kongamano la Nne la Idhaa za Kiswahili Duniani linalofanyika katika Hoteli ya Eden Highlands jijini Mbeya.

Amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua kadhaa ili kukibidhaisha Kiswahili na moja ya hatua hizo ni kuandaa Mkakati wa Taifa wa kubidhaisha Kiswahili ambao una lengo la kuifanya lugha hiyo kuwa bidhaa kwa kutoa fursa za kujikwamua kiuchumi kwa rasilimaliwatu wanaojihusisha nayo pamoja na watoa huduma za kiswahili.

Amesema Serikali imeendelea kuhakikisha balozi zetu zinakuwa kitovu cha kueneza Kiswahili katika nchi za ughaibuni, ili kufanikisha azma hiyo, Serikali imeratibu ufunguzi wa vituo vipya vya kufundisha Kiswahili katika balozi mbalimbali za Tanzania ughaibuni. Miongoni mwa nchi hizo ni Uholanzi, Falme za Kiarabu za Kiarabu na Dubai, Ujerumani, Italia, Zimbabwe, Nigeria, Comoro, Ufaransa, Korea na Uturuki.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameelekeza kuwa nyaraka za mawasiliano za wizara, idara na taasisi zake ziandikwe kwa Kiswahili sanifu, vilevile, mikutano, warsha, dhifa, semina na mijadala ya umma iendeshwe kwa lugha ya Kiswahili.

“Sheria, kanuni, miongozo na mipango mkakati ambayo bado haijatafsiriwa kwa Kiswahili, itafsiriwe kwa kushirikiana na Mabaraza ya Kiswahili (BAKITA na BAKIZA) na watalaamu wengine wa Kiswahili.”alieleza

Pia ameielekeza BAKITA na BAKIZA waandae na kutekeleza mpango wa mafunzo kwa makundi mbalimbali kama vile wahariri, wafasiri, wakalimani, waandishi wa vitabu, walimu, makatibu muhtasi, washereheshaji na makundi mengine mengi yanayotumia na kukieneza Kiswahili.

“…Shirika la Viwango Tanzania, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba shirikianeni na BAKITA, BAKIZA pamoja na wataalamu wengine wa Kiswahili kutafsiri kwa Kiswahili maelekezo ya bidhaa na huduma zinazotolewa na wadau mbalimbali.”

Akizungumzia kuhusu lengo la kongamano hilo pamoja na mambo mengine amesema linalenga kujadiliana kuhusu maudhui ya utangazaji kwa kutumia lugha ya kiswahili na kutambua jitihada za vyombo vya habari katika kukifanya kiswahili kuwa bidhaa.

“Kiswahili ni utambulisho wa taifa letu na wote tunatambua mchango mkubwa wa Kiswahili katika uhuru wa Tanganyika, Mapinduzi ya Zanzibar na harakati za ukombozi katika bara letu la Afrika.”

Waziri Mkuu amesema kaulimbiu ya kongamano hilo inasema “Tasnia ya Habari na Fursa za Ubidhaishaji wa Kiswahili Duniani”, ambayo kimsingi inaweka msisitizo kuhusu nafasi ya tasnia ya habari katika kukinadi na kukieneza kiswahili duniani. “Kwa upande mwingine, inaweka msisitizo katika nafasi kubwa waliyonayo wanahabari kwa maendeleo ya lugha ya Kiswahili.”alisema

Amesema kaulimbiu hiyo ni utekelezaji wa vitendo wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020/2025, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano Awamu ya Tatu, Dira ya Maendeleo ya Taifa Mwaka 2025, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar Mwaka 2050 pamoja na Mpango wa Maendeleo ya Zanzibar Mwaka 2021-2026.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan (wakati akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) kwenye ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili yaliyofanyika Jijini Dodoma, mwezi Januari, 2021 alielekeza Wizara zinazohusika na utamaduni nchini, zibaini maeneo ambayo bado Kiswahili hakitumiki ipasavyo ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.

Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais, alitoa maelekezo kwa mabaraza ya Kiswahili yaandae mikakati mahususi ya kukikuza na kukiendeleza Kiswahili ili Serikali iyawezeshe kwa kuyapatia wataalamu na itenge fedha katika bajeti kwa ajili ya miradi ya Kiswahili ya mabaraza haya.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Tabia Maulid amesema kwa kushirikiana na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania Bara, Dkt. Damas Ndumbaro watahakikisha lugha ya kiswahili inaendelea kukua kimataifa na kuwa bidhaa muhimu katika kukuza uchumi na kuvutia utalii nchini.

Naye, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Ndumbaro ametumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa aliyoyafanya katika wizara yao katika kipindi cha miaka mitatu tangu Serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani.

“…Katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ametuwezesha kufungua vituo 44 vya kufundisha kiswahili na tumeona faida yake. Vyombo vya habari 44 vinatangaza kwa kiswahili duniani na hivyo kukiwezesha kiswahili kuzidi kukua na kupendwa duniani na kuongeza fursa za ajira kwa wahariri, walimu na wakalimani.”

Akizungumzia kuhusu kongamano hilo, Dkt. Ndumbaro amesema lugha ya kiswahili kwa sasa imekuwa bidhaa inayouzika kwa kasi kubwa duniani na Tanzania imeendelea kukuza lugha hiyo kupitia utamaduni, sanaa na michezo kupitia nyimbo na shughuli mbalimbali za kimichezo na utamaduni.

Awali, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Consolata Mushi alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa jitihada za kukibidhaisha Kiswahili na kuziagiza balozi za Tanzania katika Mataifa mbalimbali kufungua madarasa ya kufundisha lugha hiyo ambapo hadi sasa vituo 16 vimefunguliwa nje ya nchi na 28 vimefunguliwa nchini.

Mapema, Waziri Mkuu alikabidhi tuzo ya heshima kwa aliyekuwa Rais wa awamu ya Pili, Hayati Ali Hassan Mwinyi ambaye alitoa mchango mkubwa katika kukuza kiswahili kwa kuhamasisha matumizi ya kiswahili sanifu, kukosoa na kuelekeza matumizi sahihi ya maneno ya kiswahili. Pia alikuwa mwenyekiti wa BAKITA (1968-1978).
Tuzo hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia BAKITA kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kupokelewa na mtoto wa marehemu Abdulla Ali Mwinyi.

About the author

mzalendo