Kimataifa

PUTIN ASHINDA UCHAGUZI MKUU URUSI KWA 88% YA KURA

Written by mzalendo

Huku kuhesabu kura katika uchaguzi wa Rais wa Urusi kukiwa kunaendelea, matokeo ya awali yanaonyesha kuwa Vladimir Putin ameshinda kwa kishindo kwa kupata takriban asilimia 88 ya kura zote za kuwania muhula mwingine wa miaka sita madarakani.

Matokeo ya mapema yaliyotolewa siku ya jana na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo yanaonyesha kuwa Putin amepata asilimia 87.8 ya kura, huku asilimia 60 ya kura zikiwa zimehesabiwa. Huu unatazamiwa kuwa ushindi mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Russia baada ya kuanguka Shirikisho la Sovieti.

Wagombea waliosalia hawajaweza kupata hata zaidi ya asilimia 5 ya kura. Mgombea wa Chama cha Kikomunisti Nikolai Kharitonov ameshinda nafasi ya pili kwa asilimia 4 ya kura.

Uchaguzi wa nane wa urais nchini Urusi ulianza Ijumaa na kuendelea hadi Jumapili. Katika mkutano na waandishi wa habari mapema Jumatatu asubuhi katika makao makuu yake ya kampeni huko Moscow, Putin aliwashukuru Warusi waliopiga kura, akisema matokeo ya uchaguzi wa rais yataruhusu jamii ya Warusi kuungana na kuwa na nguvu zaidi.

Ameongeza kuwa ushindi wake katika uchaguzi wa rais unaonyesha Warusi wamekuwa na imani na uongozi wake.

Rais wa zamani wa Urusi, Dmitry Medvedev, amempongeza Putin kwa ushindi wake katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.

“Ninampongeza Vladimir Putin kwa ushindi wake mkubwa katika uchaguzi,” Medvedev amesema kwenye Telegram.

Kulingana na maafisa wa uchaguzi, waliojitokeza kupiga kura nchini kote walifikia asilimia 74.22 na hivyo kupita viwango vya 2018 wakati asilimia 67.5 walijitokeza kupiga kura.

Putin aliteuliwa kwa mara ya kwanza kama kaimu rais mwaka 1999 wakati Rais wa zamani wa Russia Boris Yeltsin alipojiuzulu. Kisha alishinda uchaguzi wake wa kwanza wa urais mnamo Machi 2000 na muhula wa pili mnamo 2004.

Baada ya awamu mbili kama rais, Putin aliteuliwa kuwa waziri mkuu mwaka 2008 ili kukwepa marufuku ya kikatiba ya kushikilia zaidi ya mihula miwili mfululizo kama mkuu wa nchi.

Lakini alirejea kwenye kiti cha urais mwaka 2012 na kushinda muhula wa nne mwaka wa 2018. Katika ya Russia ilibadilishwa mwaka 2020 na kuongeza mihula ya urais na kwa msingi huo Putin anaweza kubakia kama rais wa Urusi hadi mwaka 2036.

About the author

mzalendo