Kitaifa

WAZIRI JAFO AWASILISHA TAARIFA YA MIRADI KWENYE KAMATI YA BUNGE

Written by mzalendo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt.
Selemani Jafo amesema miradi mbalimbali ya mazingira imechangia
kuwajengea wananchi uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya
tabianchi.

Ametoa kauli hiyo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa
Urejeshwaji wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR)
unaotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa pamoja na taarifa ya
utekelezaji wa Mradi wa Hifadhi Endelevu ya Ardhi katika Bonde la Ziwa Nyasa
(SLM-Nyasa) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira katika
kikao kilichofanyika leo Machi 12, 2024 jijini Dodoma.

Dkt. Jafo amesema kuwa kutokana na wananchi kuendelea kupata elimu ya
mazingira, wameendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za upandaji wa
miti hatua iliyochangia kupatikana kwa mvua katika maeneo mbalimbali nchini.
“Mheshimiwa Mwenyekiti kupitia Kamati yako mmefanya kazi kubwa sana
kwani mmetupa maelekezo ambayo tumeyafanyia kazi hasa katika eneo la
kuwaelimisha wananchi kuhusu kuhifadhi mazingira na matunda yake
tunayaona, wananchi wengi wameendelea kupanda miti kwa wingi,”
amesema.

Dkt. Jafo amesema kuwa kutokana na uharibifu wa mazingira katika bonde la
Ziwa Nyasa unaotokana na shughuli za kibinadamu zisizo endelevu, Ofisi ya
Makamu wa Rais inatekeleza Mradi wa SLM-Nyasa kuwajengea uwezo
wananchi hao kutumia mbinu bora za kuhifadhi ardhi.

Ameongeza kuwa kupitia mradi huo wananchi wanaojengewa uwezo
wanaweza kuboresha maisha yao kwa kuwa na njia mbadala ya kujipatia
kipato na kuachana na vitendo vya ukataji wa miti ovyo au uvuvi usio
endelevu.

Halikadhalika, Waziri Dkt. Jafo amesema Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza
Mradi wa SLR ili kuimarisha usimamizi jumuishi wa mazingira na urejeshwaji
wa mazingira yaliyoharibiwa ili kujenga uhimilivu wa mifumo ikolojia.

About the author

mzalendo