Na: OWM – TAMISEMI, Dodoma
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Dkt. Jafar Seif, amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwekeza katika miradi ya maendeleo yenye tija na manufaa kwa wananchi, hususan katika kuimarisha utoaji wa huduma bora za kijamii kupitia ujenzi wa miundombinu imara ya barabara, afya ya msingi na elimu ya msingi.
Dkt. Seif ametoa wito huo leo, Agosti 19, 2026, kwa viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa niaba ya Waziri wa Nchi, OWM–TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 16 wa Mwaka wa Taasisi ya Maboresho katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA), unaofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 21 Agosti, 2026 katika Ukumbi wa Jiji, uliopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Seif amesema kaulimbiu ya mkutano huo, isemayo “Ugatuzi wa Madaraka katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni Nguzo Madhubuti ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” inapaswa kuwa chachu kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwekeza katika miradi yenye tija, kuimarisha na kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani, kutoa huduma bora kwa kuzingatia mahitaji ya jamii na kuhakikisha matumizi sahihi ya fedha za umma.
“Maendeleo ya Taifa letu yanategemea uwezeshwaji wa wananchi katika ngazi ya msingi. Hivyo, mnao wajibu wa kuendelea kuimarisha misingi ya ugatuzi wa madaraka kwa vitendo, ili wananchi waone matokeo halisi katika maisha yao ya kila siku,” amesema Dkt. Seif.
Aidha, Dkt. Seif amewataka washiriki wa mkutano huo wa TOA kuyaishi kwa vitendo maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea wananchi tabasamu kwa kuwapatia huduma bora na kwa wakati, pamoja na kuwa nuru na mwanga halisi katika kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu, kama ambavyo Mhe. Rais amekuwa mstari wa mbele.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TOA, Bw. Albert Gabriel Msovela, amemhakikishia Dkt. Seif kuwa taasisi hiyo, kupitia malengo yake makuu, itaendelea kushirikiana na Serikali katika kusimamia maendeleo ya wananchi na kuimarisha utawala bora.
Bw. Msovela ameongeza kuwa TOA imejipanga kimkakati kuhakikisha inatoa mchango katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Zanzibar (ZALGA), Dkt. Mohammed Makame Mohammed, amesema ushiriki wao katika mkutano huo utatoa fursa ya kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano, jambo litakalowezesha utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Zanzibar na Tanzania Bara.
Mkutano huo Mkuu wa 16 wa Mwaka wa TOA unahudhuriwa na Makatibu Tawala wa Mikoa yote 26, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, zikiwemo Jiji, Manispaa na Halmashauri, pamoja na Makatibu Tawala wa Wilaya zote 136 nchini.
