Uncategorized

SERIKALI KUIOMBA UNESCO KIBALI KUTENGENEZA BARABARA ZA LAMI,ZEGE HIFADHI YA SERENGETI

Written by mzalendo
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Machi 10,2024 jijini Dodoma  kuhusu maendeleo ya utalii na miundombinu baada ya mvua kunyesha kwenye hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ipo chini ya Mamlaka za hifadhi za Taifa (TANAPA).
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi, akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 10,2024 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
SERIKALI  kwa kushirikiana na Mamlaka za hifadhi za Taifa (TANAPA) inaandaa andiko la kitaalam la kuwasilisha kwenye  Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuhusiana na suala la  kukarabati barabara  kwa kiwango cha zege na lami katika hifadhi ya Serengeti.
Hatua hiyo ni kutokana na Mvua zinazoendelea kunyesha za El Nino ambazo zimeleta athari ya uharibifu wa miundombinu ikiwemo barabara za kwenye hifadhi za taifa zilizo chini ya TANAPA
Hayo yamebainishwa leo Machi 10,2024 jijini na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya utalii na miundombinu baada ya mvua kunyesha kwenye hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ipo chini ya TANAPA.
Amesema njia ya kutumia andiko la kitaalam ndiyo iliyotumiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya
Eneo la Ngorongoro (NCAA) ambapo sasa imepata kibali cha kujenga barabara
yenye tabaka gumu na kufafanua kuwa barabara hiyo ndiyo ndiyo inayoingia hifadhini Serengeti kwa  kuzingatia kuwa vivutio hivi viwili maarufu duniani vinapakana.
“Kuna barabara kuu nne zenye changamoto zaidi kutokana na upitaji wa magari
makubwa ya abiria na mizigo yanayokwenda mikoa ya jirani ya Mara, Arusha,
Manyara, Mwanza, Shinyanga na Simiyu ambazo TANAPA ndizo inazozilenga
katika mkakati wake wa mbinu mbadala ya tabaka gumu iwapo itakubalika, “amesema Bw.Matinyi
Amesema kutokana na mvua hizo tayari TANAPA katika hatua za awali tayari imekamilisha matengenezo ya barabara  na sasa barabara hizo zinapitika na watalii wanaendelea kupata huduma  zinazostahili.
Amesema Serengeti ni hifadhi ya Taifa ambayo inaliingizia Taifa fedha nyingi kwa kuwa watalii wengi hupenda kutembelea hifadhi hiyo kwa ajili ya kujionea wanyama wakubwa duniani na uhamaji wa wanyama aina ya nyumbu kwenda nchini Kenya na kwamba imechukua tuzo ya hifadhi bora Afrika kwa miaka mitano mfululizo.
 “Hifadhi hiyo imeingiza watalii 1,451,176 kwa miezi nane pekee kutoka ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi Februari 2024 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo lengo lilikuwa ni kufikisha watalii 1,387,987 hivyo lengo hilo limevukwa kwa kipindi cha miezi nane tu.”amesema Matinyi

About the author

mzalendo