Kitaifa

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YAPONGEZA JUHUDI ZA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA

Written by mzalendo

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ikitembelea na kukagua Kliniki ya Methadone iliyopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala wakati wa ziara ya Kamati hiyo Jijini Dar es salaam.

Na Mwandishi wetu- Dar es salaam

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria yaridhishwa na juhudi zinazoendelea nchini za kuthibiti dawa za kulevya.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama wakati ilipotembelea Kliniki ya Methadone iliyopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala pamoja na Ofisi za Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Jijini Dar es salaam.

Dkt. Mhagama alisema kuwa, kiwango cha dawa za kulevya kinachokamatwa kwa sasa ni mara nne ya kilichokuwa kikikamatwa awali hatua iliyotokana na kuongezeka kwa juhudi za ukamataji.

“Kuongezeka kwa idadi ya dawa za kulevya zinazokamatwa nchini haimaanishi kwamba uuzaji na uingizaji wa dawa hizi umeongezeka bali inamaanisha kuwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imeongeza nguvu katika kuthibiti” Alisema Dkt. Mhagama.

Alitumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama, pamoja na timu yake katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya hali ambayo inaonyesha dhahiri kuwa Watanzania wapo salama.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya uwekezaji mkubwa katika kuhakikisha kuwa biashara za dawa za kulevya inadhibitiwa nchini,”Alisema.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. Jenista Mhagama alieleza kuwa, serikali inatambua tatizo linalowapata waraibu wa Dawa za kulevya ambapo Serikali imeweka programu ya dawati tiba mbadala wanayoipata warahibu na itaendelea kuongeza vituo vingi ili waraibu wengi wapate matibabu.

“Kwa sababu waraibu wakipona wakawa hawana shughuli za kufanya ni rahisi kurudi kule walipotoka hivyo kama Serikali tutajitahidi kuwapatia kazi mbadala ya kuwaingizia kipato,” Alisema Mhagama.

Naye Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo alibainisha kwamba waraibu kwa sasa wamepungua katika maeneo mbalimbali zikiwemo vituo vya usafiri na mitaani kutokana udhibiti wa dawa hizo kuongezeka.

About the author

mzalendo